1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshirika wa Trump alikiuka kikwazo cha silaha Libya

Josephat Charo
23 Februari 2021

Umoja wa Mataifa unasema mshirika wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump na kampuni tatu za Umoja wa Falme za Kiarabu zilikiuka vikwazo vya silaha dhidi ya Libya. Prince ni muasisi wa kampuni ya ulinzi ya Blackwater.

https://p.dw.com/p/3pl8f
UN-Sicherheitsrat New York 2016 | Waffenembargo Libyen
Picha: Imago Images/Xinhua

Mkandarasi wa Kimarekani, Erik Prince, ambaye ni mshirika wa karibu wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, alikiuka kikwazo cha silaha cha Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya, pamoja na kampuni tatu katika Umoja wa Falme za Kiarabu na mameneja watatu, wakati wa operesheni ya kumsaidia kamanda muasi wa kijeshi kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Katika sehemu muhimu ya ripoti ya baraza la usalama iliyopatikana na shirika la habari la Associated Press Jumamosi iliyopita, jopo la wataalamu liliorodhesha operesheni maalumu ya kampuni ya kibinafsi ya kijeshi iliyopewa jina Project Opus, iliyonuiwa kumpelekea silaha na vifaa vya kijeshi kamanda wa serikali ya mashariki ya Libya, Khalifa Haftar. Mpango huo pia ulijumuisha kuwateka nyara au kuwaua watu waliochukuliwa kuwa hatari Libya.

Prince pamoja na mwanamume mwingine aliyetajwa katika ripoti hiyo amekanusha kuhusika kufanya makosa. Operesheni hiyo iliripotiwa mara ya kwanza na magazeti ya New York Times na Washington Post.

Haftar alitakiwa kupewa ndege za kivita

Ripoti ya jopo la watalaamu wa Umoja wa Mataifa imesema iliigundua operesheni ya Project Opus mnamo Juni 2019. Ilinuiwa kuziruhusu kampuni binafsi za kijeshi kuvipa vikosi vya Haftar ndege za kivita, ndege zenye mifumo ya kukusanya taarifa za kijasusi, uwezo wa kuzuia mashambulizi upande wa baharini, mtandaoni na nyenzo za kulenga shabaha.

Kuba Fluggesellschaft Aerogaviota Antonow AN-26B
Picha: Imago/R. Peters

Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, Prince alianza kushiriki wakati maafisa wa Jordan walipofahamu vipengee vya mpango huo na kusitisha mnada wa helikopta za kijeshi kwa Haftar mnamo Juni 2019. Helikopta tatu zilikuwa ziagizwe kutoka kwa kampuni moja ya Afrika Kusini na moja kutoka Umoja wa Famle za Kiarabu. Pia ndege chapa Antonov AN-26B kutoka kwa kampuni ya Bermuda, ndege chapa LASA T-Bird kutoka kwa kampuni ya Bulgaria na ndege chapa Pilatus T-Bird ISR kutoka kwa kampuni ya Austria.

Uchunguzi zaidi wa jopo umebaini Erik Prince alipendekeza operesheni hiyo kwa Khalifa Haftar mjini Cairo mnamo Aprili 14, 2019 na kwa hiyo imemkuta Prince na hatia ya kuvunja azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 lililoiwekea Libya kikwazo cha silaha. Gazeti la Washington Post limeripoti kwamba wakili anayemtetea Prince, Matthew Schwartz, amesema mteja wake hajavunja sheria yoyote.

Prince, muasisi wa kampuni ya ulinzi ya Blackwater, alipata umaarufu baada ya wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwapiga risasi na kuwaua raia 17 wa Iraq katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad wakati wa vita vya Iraq.

Wataalamu hao pia wamesema Umoja wa Famle za Kiarabu haikutoa ushirikiano kwa jopo hilo, haijajibu maombi ya kutoa taarifa na majibu kutoka Jordan na Afrika Kusini yalitoa taarifa chache sana kinyume na jopo lilivyokuwa limeomba.