1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshirika wa kansela Angela Merkel afungishwa virago!

26 Septemba 2018

Bwana Volker Kauder kiongozi wa wabunge wa vyama viwili vya CDU na CSU, ameshindwa katika uchaguzi wa ndani wa chama cha CDU. Matokeo ya uchaguzi huo yaliyowashangaza wengi yanazingatiwa kuwa onyo kwa Kansela  Merkel. 

https://p.dw.com/p/35WKs
Unionsfraktion im Bundestag, Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) und Volker Kauder (CDU)
Picha: picture-alliance/dpa/K.Nietfeld

Hatma ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel imegonga vichwa vya habari za kitaifa juu Jumatano ya leo wakati chama chake kikiyakataa mapendekezo ya kwamba kufanyike kura ya kutokuwa na imani dhidi ya bibi Merkel bungeni. Kiongozi mpya wa bunge aliyechaguliwa amesema mapendekezo ya chama cha upinzani chakiliberali cha FDP hayana msingi.

Katika kura ya ndani ya chama cha CDU iliyowashangaza wengi Bwana Volker Kauder aliyekuwa kiongozi wa wabunge wa chama hicho bungeni, kwa muda wa miaka 13 aliangushwa katika uchaguzi huo wa ndani na naibu wake Ralph Brinkhaus. Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza kwa Kauder kusimama katika uchaguzi dhidi ya mshindani mwengine.

Ralph Brinkhaus kiongozi mpya wa wabunge wa vyama vya CDU/CSU bungeni
Ralph Brinkhaus kiongozi mpya wa wabunge wa vyama vya CDU/CSU bungeniPicha: picture-alliance/Eventpress Stauffenberg

Katika kura hiyo ya siri naibu wake huyo Brinkhaus alipata kura 125 wakati yeye aliambulia kura 112.  Bwana Ralph Brinkhaus sasa  atakuwa kiongozi wa wabunge wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union - CDU na Christian Social Union- CSU. Bwana Brinkhaus amesema atatoa  mchango madhubuti katika serikali ya mseto ya vyama vya CDU,CSU na SPD. Pia ameeleza wazi kwamba kushiriki kwake katika kinyang'anyiro cha uchaguzi siyo ishara ya kumwendea kinyume kansela Angela  Merkel. 

Hata hivyo wachambuzi wengi wa kisiasa wanazingatia kuchaguliwa kwa bwana Brinkhaus kuwa ni uasi wa kiasi fulani na wamesema kuwa kura hiyo ni ishara dhahiri kwamba kansela Merkel anazidi kupoteza idadi ya wanaomuunga mkono ndani ya vyama  vya  kihafidhina vya CDU na CSU.

Viongozi muhimu wa vyama hivyo ikiwa pamoja na waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer na kiongozi wa chama CSU katika jimbo la Bavaria Alexander Dobrint walijaribu kutoa mwito kwa wanachama wengine wa kumuunga mkono bwana Kauder aliyeshindwa  katika uchaguzi huo.

Volker Kauder aliyekuwa kiongozi wa wabunge wa vyama vya CDU/CSU bungeni
Volker Kauder aliyekuwa kiongozi wa wabunge wa vyama vya CDU/CSU bungeniPicha: picture-alliance/M.Schreiber

Hata hivyo, katika tamko lake baada ya kufanyika uchaguzi huo Kansela Merkel alimpongeza mshindi  bwana Brinkhaus na kuhahidi kufanya kazi naye kwa kadri itakavyowezekana. Pia alimshukuru bwana Kauder  kwa kazi ya  miaka mingi aliyofanya. 

Juu ya kushindwa kwa bwana Kauder, kiongozi wa chama cha mrengo mkali wa kulia bungeni, AfD, Alice Weidel, amesema Kansela Merkel yumo katika hali ya kutumia nguvu zake za mwisho! Weidel amesema matokeo hayo ya kura yanaonyesha kuwa Kansela Merkel hakidhibiti tena chama chake.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPA/p.dw.com/p/35U0E

Mhariri: Mohammed Khelef