1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Vyombo vya habariAfrika

Tobore Ovuorie: Sikuchulii hapana kuwa jibu

15 Juni 2021

Mshindi wa tuzo ya uhuru wa habari ya DW Tobore Ovuorie amehatarisha maisha yake kama mwandishi wa habari za uchunguzi. Anazungumzia madhara ya muda mrefu ya uchunguzi wake, uhuru wa kujieleza na mipango yake ya baadae.

https://p.dw.com/p/3uyDB
DW Freedom of Speech Award Laureate 2021: Nigerian investigative journalist Tobore Ovuorie
Picha: Philipp Böll/DW

Mwandishi habari wa Kinigeria Tobore Ovuorie alishinda tuzo ya DW ya Uhuru wa Kuzungumza ya mwaka 2021 kwa kujiotoa kwake kupigania haki za binaadamu na uhuru wa kujieleza nchini Nigeria. Anajulikana zaidi kwa kazi yake ya kufichua genge za usafirishaji haramu wa binaadamu mwaka 2013, wakati ambapo alidhalilishwa, kubakwa na karibu kuuawa.

"Leo, tunamtunza mwandishi shupavu kutoka Nigeria," alisema Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg siku ya Jumatatu. "Tobore Ovuorie amekutana na changamoto kali wakati wa uchunguzi wake dhidi ya usafirishaji haramu wa wanawake vijana kutoka Afrika kwenda Ulaya. Alivutia nadhari ya mamlaka kuhusu hatma ya maelfu ya wahanga, ambao, bila kazi ya mwandishi huyu jasiri, wasingelazimika kuchukuwa hatua."

'Leta mwanga palipo na giza'

Wakati akikubali tuzo hiyo mjini Bonn, Ovuorie alizungumzia changamoto ambazo waandishi wanakabiliana nazo nchini mwake. "Kuwa mwandishi nchini Nigeria ni ngumu. Tunapigania msingi wa kiuchumi kwa kazi yetu na kupigania upatikanaji wa taarifa. Tunawekewa vikwazo tunapouliza maswali na kudhalilishwa, kutishiwa, kukamatwa na kufungwa," alisema Ovuorie. "Naweza kusema kwa kujiamini kwamba uhuru wa habari nchini mwangu na mataifa jirani kama Cameroon, uko katika hali mbaya."

DW Freedom of Speech Award Laureate 2021: Nigerian investigative journalist Tobore Ovuorie
Mshindi wa tuzo ya uhuru wa habari ya DW Tobore ovuorie.Picha: Philipp Böll/DW

Soma pia: Tobore Ovuorie atunukiwa tuzo ya DW ya Uhuru wa kujieleza

Mshindi huyo wa Tuzo ya Uhuru wa Habari ya DW pia aliitolea wito serikali ya Nigeria kuunga mkono uhuru wa kujieleza na kuondoa marufuku yake dhidi ya mtandao wa kijamii wa Twitter. "Natumia fursa hii kuzitolea mwito serikali mbalimbali za ulimwengu kuisihi serikali ya Nigeria kukomesha marufuku yake dhidi ya Twitter. Demokrasia inapaswa kuwa ya watu na kwa ajili ya watu. Siyo chini ya hapo," alisema.

Ovuorie pia aliwasihi waandishi wenzake duniani kushikilia mapambano yao ya kufichua dhulma ndani ya jamii zao. "Kwa vyovyote vile hatupaswi kuacha sauti yetu inyamazishwe. Lazima tukatae kuwatii madikteta. Kwa namna hiyo, tutaleta mwanga katika giza na jamii zetu mbalimbali na mataifa yatakuwa maeneo makini zaidi, salama zaidi na bora zaidi kwetu sote na vizazi vijavyo."

Mwandishi wa DW, Mimi Mefo Takambou, alizungumza na Tobore Ovuorie kuhusu athari za muda mrefu za uchunguzi wake, uhuru wa kujieleza nchini mwake na mipango yake ya baadae.

DW Freedom of Speech Award Laureate 2021: Nigerian investigative journalist Tobore Ovuorie
Mwandishi wa habari za uchunguzi wa Nigeria Tobore OvuoriePicha: Philipp Böll/DW

Mahojiano na Tobore Ovuorie

DW: Serikali ya Nigeria imepiga marufuku matumizi ya mtandao wa Twitter nchini kote. Ni upi mtanzamo wako kuhusu hilo?

Tobore Ovuorie: Nadhani marufuku ya serikali ya Nigeria dhidi ya Twitter imepotoka. Nadhani serikali inawekeza nguvu katika mwelekeo usio sahihi kwa sababu sasa hivi tuna hali mbaya ya usalama nchini. Kwenye barabara kuu, wasafiri wanatekwa na wazazi wao kulazimishwa kulipa mamilioni ya naira kama kikomboleo. Tuna mzozo wa wafugaji wa kabila la Fulani.

Soma pia: Dunia yaadhimisha uhuru wa vyombo vya habari

Ni vurugu moja kwenda nyingine. Ukiwa na yote haya akilini, kuja na marufuku ya Twitter, ni jambo lililoshauriwa vibaya. Iwapo nguvu inayowekezwa kwenye marufuku ya Twitter iliwekezwa katika kukabiliana na ukosefu wa usalama au hata suala la ugavi wa umeme nchini, nadhani serikali ingepata mafanikio makubwa na Nigeria ingekuwa bora. Hivyo marufuku ya Twitter - ni 'hapana' kwangu.

DW: Wengi wanahofia marufuku ya Twitter itakuwa na madhara kwa waandishi habari. Hasa wale wenye simulizi za kuvutia kama wewe. Unadhani madhara hayo yatakuwaje?

Siyo waandishi tu watakaohisi madhara ya marufuku hii. Nawafahamu Wanigeria wengi waliotumia muda mrefu kutafuta ajira lakini hawakuweza kupata kazi. Hivyo walianzisha biashara ndogo ndogo. Nimekuwa mteja wa baadhi ya vijana hao. Unajua, nakuja Twitter, naona wanachokitangaza. Nakipenda na mara moja nakwenda kwenye tovuti zao, tunafanya biashara. Kwa kupigwa marufuku Twitter, vijana hao, njia yao ya kuingiza kipato imefungwa. Hakuna ajira, hakuna njia ya kufanya biashara. Hivyo nini kinafuata kwao?

Kama mwandishi wa habari, natumia Twitter kujua habari zinazovuma kwenye mitandao na mengine. Tangu marufuku hiyo, nahisi kama mwizi anayejipenyeza kwenye nyumba yangu mwenyewe. Unajua, nalazimika kutumia VPN na baadhi ya mitandao hii ya VPN, huwezi kuiamini sana.

DW: Wewe ni mmoja wa wachunguzi wa siri. Miongoni mwa mambo mengine, ulifichua genge la kimataifa la usafirishaji haramu wa binaadamu kwa kujifanya kama kahaba. Nini kilikuwa kinaendelea kichwani mwako wakati wa uchunguzi huo?

Hususani, kuelekea awamu ya mwisho ya uchunguzi, mambo yalikwenda mrama kweli. Kulikuwa na wakati nililazimika kuvua - na ninaposema kuvua, sikuwa nimevaa chupi au sidiria. Nilijiskia vibaya. Nilihisi kugeuzwa kielelezo cha uthibitisho. Na hilo lilikuwa na athari hasi kwangu. Hatimaye nilipoondoka kwenye eneo hilo, nilienda tu nyumbani. Muda uliosalia kwenye siku yangu ulikuwa umevurugwa. Nilioga na kulia vibaya bafuni na kisha nikaenda kulala. Sikuweza kufanya kitu kingine siku hiyo. Lakini hicho siyo kitu pekee kilichotokea. Nilipewa kitu cha kuvuta. Nina matatizo ya pumu, hivyo sipendi masuala ya kuvuta kabisa. Na niliishia kukumbwa na pumu, nilikimbizwa hospitali ambako niliwekwa kwenye oksijeni. Kusema kweli, nilikuwa naomba tu kwamba nitoke nikiwa hai.

DW: Nini kilikusukuma kufanya uchunguzi huu?

Kilichonipa nguvu kuendelea ni kwamba nilimpoteza mtu wa karibu sana kwangu kwa usafirishaji haramu. Sikuwa na fursa ya kuzungumza naye kabla ya kufariki. Hivyo hii ilisababisha hasira ndani yangu. Kisha, mbali na ukweli kwamba niliathiriwa binafsi, huwa sikubali kushindwa. Wakati ninaposema sawa, nakwenda kufanya hili, napenda kuhakikisha kwamba nalifikisha mwisho. Ikiwa unaniambia hapana, upende usipende, utanikubalia ombi langu. Sikubali kukatiwa nitakalo.

DW: Kama mwanamke mwandishi wa habari za uchunguzi katika nchi kama Nigeria, umeweza kuweka urari kati ya kazi yao na usalama wako binafsi?

Kwanza kabisaa, ngoja nisisitze, ni kazi kuwa Mnigeria. Kisha, kuwa mwandishi habari za uchunguzi ni kazi ya ziada. Lakini mwandishi mwanamke wa habari za uchunguzi ni kazi ya ziada. Hata kabla ya uchunguzi, nilikuwa nimejifunza kuchukuwa tahadhari, lakini uchunguzi huu hasa ulifanya mambo kuwa mabaya zaidi. Nakumbuka kulikuwa na wakati nilikwenda kutafuta nyumba na kulikuwa na eneo hili zuri la makaazi. Nilimuuliza meneja, kuna njia nyingine za kutoka mbali na lango kuu? Na akasema: Hapana, huu ndiyo mlango pekee wa kuingia na kutoka. Na nikasema: Sitaki tena. Naona nyumba ni nzuri, lakini siwezi kuishi katika eneo ambako kuna lango moja tu. Ni kama vile naishi maisha ya utoro.

DW: Unaweza kufanya tena uchunguzi kama wa genge la usafirishaji haramu wa binadamu huko mbeleni?

Labda niseme hivi: Bila kujali kila kitu kilichotokea 2013, unajua, ubakaji, udhalilishaji wa hali ya juu, kulazimika kupambana, kuendelea kuwa kwenye matibabu. Kuna siku nahisi nzito sana hata hadi leo. Kuna siku najisikia kama mpuuzi, najisikia vibaya. Naweza kusema kama ningepata fursa ya kufanya  habari hii au kufanya uchunguzi wa usafirishaji binadamu tena: Ndiyo, naweza kuifanya tena. Nitakuwa mwangalifu zaidi kwa kuwa nina uzoefu mkubwa sasa. Nitakuwa mwangalifu zaidi. Na ngoja nikupe siri kidogo: Kuna jambo linaendelea katika mwelekeo huo.

Mhariri: Mohammed Khelef