1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msako dhidi ya wahamiaji wazua taharuki Marekani

15 Julai 2019

Wahamiaji wasiokuwa na vibali vya kuishi Marekani wameingiwa na wasiwasi toka Jumapili kufuatia zoezi la kuwasaka nchi nzima kwa amri ya rais Donald Trump.Mexico imeahidi kuwaunga mkono raia wake watakaorudishwa

https://p.dw.com/p/3M5i1
USA Razzien gegen Migranten in Texas
Picha: picture-alliance/Zumapress/C. Reed

Nchini Marekani hofu imetawala kwa wahamiaji wanaoishi katika nchi hiyo kufuatia kutangazwa msako wa nchi nzima wa kuwatafuta wahamiaji wanaoishi bila kibali wiki hii. Makanisa chungunzima  jumapili yalitangaza kuacha milango wazi kuzipokea familia za wahamiaji.

Jumapili ilikuwa siku ya hofu kubwa kwa maelfu ya wahamiaji wasiokuwa na vibali nchini Marekani waliosubiri kwa wasiwasi mkubwa zoezi la kuogofya la msako wa nchi nzima la kuwakamata na kuwarudisha makwao wahamiaji.

USA | ICE | Razzien gegen Menschen ohne Aufenthaltsgenehmigung |  Protest
Picha: picture-alliance/dpa/J. Motal

Hili ni zoezi ambalo rais wa Marekani Donald Trump aliahidi kulitekeleza  ingawa hakuna dalili za mara moja zilizojitokeza kuhusu kufanyika kwa zoezi hilo kwa kiwango kikubwa.

Hata baada ya vyombo vya habari kuripoti kwamba zoezi hilo linaendelea rais Trump alichochea mjadala mkali kuhusu suala hilo tete la uhamiaji kwa ujumbe wake wa Twitta uliosema kwamba baadhi ya wabunge wanawake kutoka chama cha Democrat wanapaswa kurudi kwenye nchi zao  zilizosambaratika kabisa na zenye uhalifu.

 Ujumbe huu wa Trump umewasirisha mno wademocrat ambapo hisia mbali mbali zimejitokeza kutoka chama hicho. Naibu spika wa bunge Mdemokrat Ben Ray Lujan aliulaani mara moja ujumbe huo wa rais akiutaja kuwa ni ujumbe wa kibaguzi dhidi ya raia wa Marekani.

Kufikia Jumapili  mawakala wa mamlaka ya uhamiaji na forodha ya Marekani ICE walitarajiwa kuendesha msako katika alau miji 10 mikubwa ya Marekani ikiweko mpango wa kuwakama takriban wahamiaji 2000 wasiokuwa na vibali vya kuishi Marekani walioingia katika nchi hiyo hivi karibuni.

USA | ICE | Razzien gegen Menschen ohne Aufenthaltsgenehmigung |  Trump
Picha: Getty Images/J. Moore

Operesheni hiyo hata hivyo imeonekana hadi wakati huu kuwa ya kiwango cha chini  kinyume na alivyotangaza Trump kutaka mamilioni wakamatwe. Pamoja na hayo pia wanaharakati walionekana wakipiga doria kwa baiskeli kwenye miji mikuu chungunzima kuorodhesha visa vya ukamataji pamoja pia na kutoa msaada kwa yoyote atakayekuwa amekamatwa.

Katika mji wa Florida walionekana maafisa wa ICE wakigonga milango, nyumba hadi nyumba, karibu na uwanja wa ndege wa Miami   kuwasaka wahamiaji.Lakini nchini Mexico nchi ambayo raia wake wengi wamehamia Mareakani ilitowa tangazo la kuwa tayari kuwapokea raia wake.Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyoMarcelo Ebrard alitowa ujumbe huu

''Wamexico watakaorudishwa  watapata fursa hapa Mexico ya ajira na uungaji mkono wa serikali ya Mexico. Tunatarajia kiasi watu 1800 lakini hatuna uhakika wa idadi itakayoingia wiki hii lakini tuko tayari kuwapokea na kuwapa ajira na kuwaunga mkono''

Ijumaa rais Trump alisistiza kwamba viongozi wengi wa miji waliunga mkono msako huo kwasababu hawataki kuwa na wahalifu kwenye miji yao.Lakini Meya wa mji wa Chicago anasema hatua hii ya wasiwasi na hofu inasababisha taharuki tu ndani ya Marekani.Viongozi wa makanisa mbali mbali wameahidi kufungua milango ya nyumba za ibada kuwahifadhi watakaoathirika na zoezi hilo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW