1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaidizi wa Merkel akosolewa kuhusu kauli yake

Sylvia Mwehozi
21 Septemba 2017

Waziri wa sheria wa Ujerumani amemshutumu mkuu wa utumishi wa kansela Angela Merkel kwa kuangukia katika mtego wa chama cha AfD baada ya kutoa kauli kwamba ni bora kutopiga kura kabisa kuliko kukichagua chama hicho

https://p.dw.com/p/2kR7f
Berlin Kanzlerin Merkel und Peter Altmaier
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Mkuu wa utumishi Peter Altmaier alijibu "ni kawaida" pale alipoulizwa swali wiki hii kuhusiana na chama mbadala kwa Ujerumani AfD. Aliongeza kwamba "AfD inaleta mgawanyiko katika nchi yetu, inatumia vibaya hofu na wasiwasi wa wananchi."

Waziri wa sheria anayefuata siasa za wastani za mrengo kushoto Heiko Maas amemkosoa mhafidhina Altmaier katika mahojiano na gazeti la Bild, akisema kuwaambia watu wasipige kura kunakisaidia chama cha AfD jambo ambalo ndilo wanalotaka.

AfD inatazamiwa kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Jumapili ambapo kiongozi mwenza Alexander Gauland pia ameikosoa vikali kauli ya Altmaier kuwa isiyo ya kidemokrasia.

Wakati hayo yakijiri Kansela Angela Merkel ambaye amerejea kutoka mahali alikozaliwa amewataka wafuasi wake kuwahimiza wapiga kura ambao hawajaamua kabla ya uchaguzi wa Jumapili na kusema hawapaswi kubweteka na matokeo ya utafiti wa maoni yanayoonyesha chama chake cha kihafidhina bado kinaongoza.

Deutschland wählt DW Interview mit Martin Schulz
Kiongozi wa SPD Martin Schulz wakati akifanyiwa mahojiano na DWPicha: DW/R. Oberhammer

Utafiti huo unaonyesha kwamba wapiga kura wengi bado hawajaamua na wakati ambapo uchaguzi unaonekana utaleta bunge lenye mgawanyiko, Merkel anataka kuongeza uungaji mkono katika nafasi yake ya kufanya majadiliano ya serikali ya pamoja.

Merkel amebainisha kwamba chama cha mrengo wa kushoto chenye msimamo wa kati cha SPD ambacho ni mpinzani wake wa karibu hakijaacha fikra ya kuunda muungano na chama cha mrengo wa kushoto na kile cha kijani muungano katika ngazi ya kitaifa.

Kiongozi wa SPD Martin schulz aliwaambia watangazaji wa kituo cha televisheni cha RTL kwamba anaamini kutakuwa na mabadiliko ya dakika za mwisho katika uchaguzi wa chama chake.

Na wakati mshale wa saa ukizidi kugonga kuelekea uchaguzi huo wa Jumapili, maafisa wa Ujerumani wamesema hakuna dalili ya mashambulizi ya mtandaoni yanayolenga kushawishi matokeo ya uchaguzi huo ingawa wameonya kwamba hawawezi kusema wako salama moja kwa moja.

Maafisa wa usalama walionya mwaka uliopita kwamba serikali ya Urusi inawza kufanya jaribio la kuyumbisha Ujerumani kwa kuhimiza vyama vya siasa kali katika uchaguzi wa Jumapili. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maizere amesema jana kwamba hawaoni rais wa Urusi Vladmir Putin akiingilia katika kampeni za uchaguzi.

Mwandishi: Sylvia mwehozi/AP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo