Msafara wa EU washambuliwa kwa bomu Somalia
1 Oktoba 2018Polisi na wafanyakazi wa huduma za dharura wamesema msafara wa magari ya kijeshi ya Umoja wa Ulaya ulilengwa na mripuko kwenye majira ya saa sita na dakika 10 mchana katika barabara ya Industrial yenye pirikapirika nyingi katikati mwa Mogadishu.
"Tumebeba maiti mbili za wenyeji na wengine wanne wamejeruhiwa," alisema Abdikadir Abdirahman kutoka shirika la huduma za kusafirisha wagonjwa la AMIN katika mazungumzo na shirika la habari la Reuters.
Polisi imesema mshambuliaji pia alifariki katika mripuko hupo. Shuhuda wa Reuters aliwaona wanaume wakilitoa gari lililoharibiwa baada ya mripuko huo kulishambulia kwa nyuma. Magari ya kijeshi yalikuwa na bendera za Italia na Umoja wa Ulaya.
Kundi la Al-Shabaab ambalo linafanya mashambulizi ya mara kwa mara katika taifa hilo la pembe ya Afrika, limedai kuhusika na mripuko huo. Jeshi la Italia limesema msafara wa magari matano yaliokuwa yanarejea kutoka shughuli ya mafunzo ulishambuliwa lakini hakuna aliejeruhiwa au kuuawa.
"Gari lililokuwa na wanajeshi wanne liliharibiwa kidogo na liliweza kurudi kambini," lilisema jeshi hilo.
Umoja wa Ulaya ni mojapo ya wafadhili wakuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM, kinachosaidia kuilinda serikali kuu ya Somalia dhidi ya waasi wa Al-Shabaab.
Somalia imekuwa katika vurugu za kivita tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990, kufuatia kupinduliwa kwa kiongozi wake Mohammed Siad Barre.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef