Msafara wa Balozi wa Uingereza Libya washambuliwa
21 Juni 2012Gari alimokuwa akisafiri balozi wa Uingereza nchini Libya limeshambuliwa kwa roketi katika mji wa Libya wa Benghazi. Walinzi wawili wa balozi Dominic Asquith walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea jana, ikiwa ni siku kadhaa baada ya bomu kuripuka nje ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini humo.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uingereza ilisema mjini London kwamba watumishi wengine wa ubalozi waliokuwa katika msafara huo walikuwa salama. Ikaongeaza kwamba maafisa wa Uingereza wanashirikiana na wenzao wa Libya kujaribu kutambuwa nani walihusika na shambulio hilo.
Wiki iliopita bomu liliripuka nje ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi bila ya kusababisha hasara yoyote. Kundi moja linalodai kupigana vita vya Jihadi, likijiita-Kikosi cha Sheikh Omar Abdulrahman, lilidai kuhusika na mashambulio hilo. Sheikh huyo kutoka Misri anatumikia kifungo cha maisha nchini Marekani kwa kuhusika katika shambulio la bomu kwenye kituo cha biashara mjini Newyork 1993.