Msaada wa Marekani kwa Waislamu Afrika
13 Julai 2004Kulingana na ripoti iliyotolewa na kikundi cha wataalamu 16, Marekani pia imeombwa kufanya jitihada mpya za kusaidia jamii ya waislamu katika Afrika.
Marekani imetakiwa kuongeza misaada ya kiuchumi kwa Afrika hasa uwekezaji, katika mataifa yanoyotoa mafuta na gesi ya eneo la magharibi, ambazo zinatarajiwa kuuzia Marekani asilimia 20 ya mafuta inayonunua kutoka nchi za nje kufikia mwaka wa 2015.
Ikiwa mataifa haya yatastawi vizuri, kuheshimu sheria, kuboresha maongozi na kutumia raslimali zao kwa busara, basi faida zitaonekana wazi ulimwenguni kote. Hivyo basi, Marekani haitakuwa na kibarua kigumu cha kudumisha ustawi, kupambana na ugaidi, kuleta maendeleo ya kijamii na demokrasia na kuhakikisha kutokuwepo kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Pendekezo la kuwasaidia waislamu linanuia kuzuia kuenea kwa upinzani wa kiislamu hasa katika maeneo ya Afrika Kazkazini, Sahel na Afrika Magharibi ambako kuna idadi kubwa ya waislamu. Ikiwa na waislamu zaidi ya milioni 300, Afrika ni mahali ambapo makundi mengi ya wanamgambo husajili wanachama wapya na pia kwa upande mwingine Marekani inapoweza kukabiliana nao.
Mpango huo utakaogharimu dola milioni 200 kwa mwaka, utaongeza pesa za misaada katika maendeleo na mipango ya elimu. Pia serikali ya Saudi Arabia itashurutishwa kuyakataza mashirika ya misaada nchini humo kutopeleka pesa Afrika, zinazohofiwa kutumika kusaidia makundi ya wapiganaji wa kiislamu.
Marekani lazima iongeze bidii katika kupunguza biashara ya silaha ndogo ndogo, kuboresha ukusanyaji wa habari na kutoa mafunzo kwa vikosi vya wanajeshi waafrika wa kulinda amani na usalama. Marekani inatakiwa kuchukua jukumu kubwa katika kuusaidia Umoja wa Mataifa katika shughuli zake za kulinda amani Afrika hasa heka heka iliyoko Sudan kwa wakati huu.
Tangu mashambulizi ya Septemba 11 mwaka wa 2001, Marekani imeongeza uhusiano wake na mataifa kadhaa ya Afrika kama vile Kenya na Nigeria. Pia imeongeza idadi ya wanajeshi wake hasa eneo la Afrika Kazkazini ambapo ilipeleka wanajeshi 2,000 huko Djibouti na katika pwani ya Afrika Magharibi.
Sudan ni nchi ambayo Marekani inaweza kuitumia kudhihirishia rasi ya Uarabuni na bara la Afrika kwamba ina moyo wa kuleta amani katika ulimwengu wote. Marekani inaweza kutumia uwezo wake wa kidiplomasia, kiuchumi na kijeshi ili kudumisha amani kati ya maeneo ya kusini na kazkazini na hasa katika eneo la Darfur. Jambo hili litaipatia sifa nzuri Marekani machoni pa waislamu.
Ripoti hiyo imeitaka Marekani kuishughulikia Somali kwani ni nchi ambayo hutumika kama makazi na njia ya wanachama wa al-Qaeda. Washington lazima ishirikiane na mataifa mengine ili kurudisha tena maongozi ya raia, huduma muhimu za kijamii na kuzima harakati za wapiganaji walio na silaha kwa kuweka vikwazo vya kuzuia biashara ya silaha.
Kuhusu uchumi, ripoti hiyo inaeleza umuhimu wa kusadia harakati za kuleta mabadiliko katika sekta ya fedha ili kuboresha uwekezaji kutoka kila upande. Mpango mpya wa Marekani uitwao Millenium Challenge Account, umesifiwa sana na ripoti hiyo. Mpango huu una dola bilioni moja zinazolenga kutoa misaada zaidi kwa mataifa ambayo yamejitolea kuleta mabadiliko katika soko la biashara, maongozi ya demokrasia, kupambana na ufisadi na kuheshimu haki za binadamu.
Mpango wa rais George Bush wa miaka mitano wa kupambana na ukimwi na matatizo mengine ya kiafya, umepongezwa sana na kikundi hicho cha wataalamu. Chini ya mpango huu, dola bilioni moja kati ya dola bilioni 15 zilizotengwa kwa matumuzi, zitapelekwa kwa hazina ya kupambana na ukimwi, malaria na kifua kikuu duniani. Hazina hii ndiyo itakayotekeleza shughuli zote za kutoa misaada kwa mataifa masikini.
Pendekezo hili limetolewa wakati ambapo Marekani inalaumiwa vikali kwa maongozi yake yasiyoshughulikia kwa dhati swala la ukimwi na kwa kupunguza idadi ya wajumbe wake kwenye mkutano unaoendelea huko Bangkok kuhusu ukimwi.