1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mrundikano wa wafungwa magerezani Tanzania washtumiwa

Hawa Bihoga DW Dar es salaam10 Februari 2020

Kituo cha sheria na haki za binadamu Nchini Tanzania kimeelezea hali ya mrundikano wa wafungwa katika magereza ya nchi hiyo, zaidi ya nusu ya wafungwa wakiwa wale ambao hawajahukumiwa.

https://p.dw.com/p/3XXp8
Maafisa wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu wakizungumza na waandishi wa habari mjiini Dar es Salaam. (Picha ya maktaba)
Maafisa wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu wakizungumza na waandishi wa habari mjiini Dar es Salaam. (Picha ya maktaba)Picha: DW/Hawa Bihoga

Kituo hicho kimeitaka wizara ya katiba na sheria ifanye mabadiliko ya sheria ili kuweka ukomo wa upelelezi wa kesi za jinai.

Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kifungu cha mia mbili ishirini na tano katika kifungu kidogo cha nne, kinatoa muda wa siku sitini kuhakikisha upelelezi unakamilika lakini kwa makosa kama vile uhujumu uchumi, uhaini na Utakatishaji fedha hayanufaiki na sheria hii.

Hatua hii inatajwa na baadhi ya wanansheria inaongeza msongamano wa mahabusu katika Magereza nchini kadhalika inaminya haki za msingi kwa watuhumiwa wa kesi mbalimbali.

Anna Henga mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu katika mkutano wake na wanahabari anasema ni wakati mwafaka kwa kwa wizara ya katiba na sheria kufanya mabadiliko ya sheria ambayo yatatoa haki ya dhamana pamoja na watuhumiwa kunufaika na kifungu cha nne kinachotoa ukomo wa siku 60 za upelelezi katika kesi za jinai.

Kituo cha sheria na haki za binadamu Nchini Tanzania kimesema asilimia 56.7 ya watu walioko magerezani nchini humo ni mahabusu.
Kituo cha sheria na haki za binadamu Nchini Tanzania kimesema asilimia 56.7 ya watu walioko magerezani nchini humo ni mahabusu.Picha: DW/S. Khamis

Kwa mujibu wa kituo hicho, asilimia 56.7 ya watu walioko magerezani ni mahabusu hivyo kupendekeza makosa yote yawe na dhamana kwa kubadilisha masharti ya dhamana kulingana na aina ya kosa Pendekezo ambalo litajwa litapunguza mlundikano wa mahabusu kwenye magereza.

Wakili Fulgenci Massawe anasema mabadiliko haya ya kutoa siku sitini kwa makosa yote, yatadumisha dhana ya mtu kutoonekana kuwa na hatia mpaka pale mahakama itakapothibitisha, hivyo haki ya mtuhumiwa kuhifadhiwa.

Sheria hii inatekelezwa kwa upande wa Tanzania bara peke, ambapo Zanzibar makosa hayo bado yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.