1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko wa Nigeria kubadili taratibu za kiusalama

29 Agosti 2011

Mripuko wa bomu uliyobomoa makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kusababisha vifo vya watu 23 katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja ijumaa iliyopita umezusha wasiwasi kuhusu hatari inayotokana na waislamu wenye itikadi kali

https://p.dw.com/p/12PGe
Majeruhi akiokolewaPicha: dapd

Kwa mujibu wa wachambuzi, vikosi vya usalama na wanadiplomasia, shambulio hilo limefanywa na Boko Haram, kundi lenye itikadi kali za kiislamu nchini humo ambapo tafsri yake "elimu ya magharibi ni haramu" Kundi hilo limedai kuhusika na mashambulio yanayaotokea takriban kila siku katika eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria pamoja na shambulio la bomu lililofanywa dhidi ya kituo cha polisi mjini Abuja mwezi Juni. Lakini shambulio dhidi ya taasisi ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa huonyesha kuwa kundi hilo linaazimia kuongeza mashambulizi yake.

Meneja wa asasi ya ushauri Druma Cussac nchini Nigeria, Peter Sharwood-Smith amesema kinachoonekana sasa ni mabadiliko katika vitendo vyao vya mashambulizi ikiwa kweli ni kundi hilo ndio lililohusika. Kutoka kuvilenga vikosi vya usalama vya nchi hiyo sasa kundi hilo limelenga kituo cha kimataifa kama jengo la Umoja wa Mataifa.

Dk. Asha Rose Migiro ni Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. alisema "Watu waliathirika si tu wanaofanya kazi hapa, lakini pia wanaokuja kwa masuala tofauti, kwa hivyo tunajua hasara yao ni hasara yetu, hasara yao ni hasara kubwa katika familia zao"

Anschlag auf ein UN Büro in Abuja Nigeria
Wanausalama wakiwa wamtanda katika jengo la UNPicha: dapd

Kundi la Boko Haram, linaloendesha operesheni zake nyingi kutoka eneo la kaskazini-mashariki, karibu na mipaka ya Cameroon,Chad na Niger, linataka sheria za Kiislamu kutumiwa kote nchini Nigeria. Kundi hilo mwaka huu, limeua zaidi ya watu 150 katika mashambulio mbali mbali.

Taarifa rasmi za upelelezi zinasema, kuna ushahidi kwamba baadhi ya wanachama wa Boko Haram, wamepata mafunzo nchini Niger na wana mahusiano na tawi la al-Qaeda katika Afrika ya Kaskazini-AQIM. Shambulio lililofanywa dhidi ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Abuja limeongeza hofu kuhusu ushurukiano huo. Shambulio hilo lilisababisha kiasi ya vifo vya watu 18, baada ya gari lililopakiwa miripuko kupita kwa nguvu milango ya kuingilia jengo hilo na kuripuka.

Juni iliyopita, kundi la Boko Haram lilifanya shambulio kama hilo katika makao makuu ya polisi mjini Abuja. Katika mashambulio yote mawili, washambuliaji walikufa lakini katika shambulio la June polisi hawana hakika kama dereva alidhamiria kujiua. Ikiwa mshambuliaji wa jengo la Umoja wa Mataifa alijitoa mhanga basi hiyo ni mara ya kwanza kwa shambulio la aina hiyo kutokea nchini Nigeria.

Kiwango cha mripuko uliotokea kwenye jengo la Umoja wa Mataifa, unaonyesha kwamba utaratibu mwingine wa mripuko ulitumika - kwa mfano, miripuko ya viwango vinavyotumiwa na jeshi kama Semtex au aina nyinginine inayotengenezwa kwa kutumia amoniaum nitrate.

Hiyo ni ishara dhahiri kwamba kati ya Boko Haram na tawi la al Qaeda - AQIM kumeanzishwa njia ya kutoa mafunzo au kusafirisha mahitaji yao.

Shambulio la pili kutokea mji mkuu katika kipindi cha miezi miwili, kutaongeza shinikizo kwa Rais Goodluck Jonathan ambae tangu aliposhika madaraka mwaka uliopita, ameeshindwa kudhibiti machafuko yanayozidi kaskazini mwa nchi hiyo. Mwezi uliopita rais huyo wa Nigeria aliunda kamati kuchunguza kiini cha machafuko katika maeneo ya kaskazini-mashariki, lakini mpaka sasa, timu hiyo inachelewesha kuwasilisha ripoti yake.

Jonathan, ni rais wa kwanza kutoka eneo la kusini la Niger Delta, lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Yeye aliibuka na ushindi katika uchaguzi uliopita, ambao wasimamizi na Wanigeria wengi wanasema ulikuwa wa haki kabisa tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi 1999.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTRE

Mhariri: Martin,Prema