Mripuko wa Ebola DRC ni wa pili mkubwa katika historia
30 Novemba 2018Mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, umegeuka janga baya la pili katika historia. Kamati ya uokozi ya Kimataifa imesema kwamba hadi kufikia sasa kumekuwa na maambukizi 426, vifo 245 huku kiwango cha vifo kikifikia asimilia 57.
Kamati hiyo ambayo ni Shirika la kibinadamu la Marekani limesema janga la Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ,limezidi kiwango cha maambukizi ya mwaka 2000-2001 cha mlipuko wa Ebola ulioikumba Uganda uliowauwa watu 224 kati ya 425 walioambukizwa, na kuwa janga la pili kubwa baada ya virusi vya ugonjwa huo kuwauwa zaidi ya watu 11,000 Afrika magharibi kati ya 2014 na 2016.
Kulipuka kwa Ebola kumetuwama zaidi Kivu Kaskazini, jimbo la Mashariki mwa Congo ambako makundi ya wanamgambo yanapigana kujaribu kudhibiti eneo hilo lenye utajiri wa mali asili.