1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko Somalia

MjahidA29 Januari 2013

Mlipuaji wa kujitoa muhanga amejiripua karibu na kasri la rais wa Somalia hii leo, na kusababisha vifo vya wanajeshi wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa. visa kama hivi mara kwa mara huwalenga viongozi nchini humo.

https://p.dw.com/p/17TK7
Mashambulizi Somalia
Mashambulizi SomaliaPicha: picture-alliance/dpa

Maasfisa wanaofanya kazi katika kasri hiyo wanasema rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, alikuwa nje ya nchi wakati wa kisa hicho na waziri mkuu wa nchi hiyo Abdi Farah Shirdon yuko salama. Rais Hassan Mohamud ameelekea mjini Brussels kwa mkutano na maafisa wa ulaya.

Mohammed Ali ambaye ni afisa wa polisi katika eneo hilo amesema mlipuaji huyo wa kujitoa muhanga alijiripua wakati alipokuwa akiulizwa maswali na askari waliokuwa katika kituo cha ukaguzi kilichokuwa mbele ya ikulu ya rais inayojulikana kama Villa Somalia. Wanajeshi wawili waliuwawa na wengine watatu wamejeruhiwa katika kisa hicho.

Jeshi la Somalia
Jeshi la SomaliaPicha: REUTERS

Askari waliokuwa katika Ikulu hiyo ambao wamekataa majina yao yatajwe, wamesema shambulizi hilo liliharibu chumba kimoja katika kasri hilo wanakoishi askari wake. Nyumba na magari yalioko karibu hayakuharibiwa.

Usalama waimarika japo kwa kiwango cha chini

Huku hayo yakiarifiwa usalama mjini Mogadishu umeimarika kiasi, tangu waasi wa Al Shabaab wanaoaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la al Qaeeda walipofurushwa katika mji mkuu huo na vikosi vya kulinda amani vya AMISOM, mwishoni mwa mwaka wa 2011.

Waasi wa Al Shabaab
Waasi wa Al ShabaabPicha: AP

Hata hivyo bado kuna visa kadhaa vya milipuko ya kujitoa muhanga na visa vya mauaji yanayodhaniwa kufanywa na waasi. Polisi kwa upande wao wamesema kumekuwa na utulivu katika mji huo na kisa cha leo ndicho cha kwanza tangu waliposhuhudia mambo kama haya katika siku ya nyuma.

Hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekiri kuhusika katika shambulizi la leo. Rais wa Somalia Sheikh Mohamud aliye na umri wa miaka 56, ambaye ni msomi na mwanaharakati kabla ya kuwa rais, anatarajiwa kuunda serikali iliyo imara zaidi tangu waasi walipoipindua serikali ya dikteta Mohammed Siad Barre mwaka wa 1991

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na waziri wa nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na waziri wa nchi za nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: Getty Images

Jamii ya kimataifa inaiunga mkono serikali ya rais wa sasa wakisema kuwa ni hatua muhimu ya kuiondoa somalia katika utawala dhaifu lakini jamii hiyo pia inakiri kuwa bado kuna mambo mengi ya kufanya ili nchi hiyo kuwa dhabiti baada ya miongo miwili ya vita. wiki iliopita Marekani iliitambua rasmi serikali ya Somalia kwa mara ya kwanza tangu kuondolewa kwa Siad Barre.

Mwandishi :Amina Abubakar/Reuters/dpa/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman