1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mripuko msikitini wauwa watu 18 Afghanistan

Daniel Gakuba
2 Septemba 2022

Mripuko mkubwa wa bomu uliotokea katika mojawapo ya misikiti maarufu nchini Afganistan umewauwa watu 18, akiwemo imamu mwenye ushawishi.

https://p.dw.com/p/4GMT0
Afghanistan Herat | Schaulustige nach Bombenexplosion
Picha: AFP

Picha zilizowekwa katika mtandao wa Twitter zimeonyesha miili ya watu iliyojaa damu, ikienea katika uwanja wa msikiti wa Gazargah kwenye mji wa Herat.

Miongoni mwa waliouwa ni Mujib ur Rahman Ansari, imam wa msikiti huo, ambaye mapema mwaka huu alipendekeza adhabu ya kukatwa kichwa kwa yeyote atakayekutwa na hatia ya kuikosea serikali, hata kama kosa ni dogo.

Visa vya vurugu vimepungua kwa kiasi kikubwa tangu Taliban walipoingia mamlakani mwaka uliopita, ingawa miripuko kadhaa ya mabomu - baadhi ikiwalenga watu wa jamii za wachache, imekuwa ikiripotiwa mnamo miezi ya karibuni. Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS limedai kuhusika na mkururo wa mashambulizi hayo.

Msemaji wa serikali ya mkoa wa Herat, Hameedullah Motawakel amesema mbali na watu 18 waliopoteza maisha, wengine 23 walijeruhiwa katika mripuko wa leo. Kifo cha Imam Ansari kimethibitishwa na msemaji wa serikali ya Taliban, Zabihullah Mujahid.

Msemaji wa Taliban amsifu imamu aliyeuawa

Kupitia mtandao wa Twitter, Mujahid amemsifu imam huyo kama ''msomi wa kidini mwenye nguvu na ujasiri, ambaye ameuawa kama shahidi katika shambulizi la kikatili.

Ansari alijulikana kwa hotuba zake kali. Kwa mfano, akihutubia mkusanyiko wa kidini mwezi Julai aliwapigia debe viongozi wa Taliban, akirai ''yeyote anayefanya kosa hata dogo dhidi ya serikali ya Kiislamu auawe kwa kukatwa kichwa.''

Ansari ni kiongozi wa pili wa kidini anayeegemea upande wa Taliban ambaye amauawa katika mripuko wa bomu nchini Afganistan katika muda usiotimia mwezi mmoja.

Shambulizi jingine kama hili lilimuuwa Rahimullah Haqqani, imam mwingine aliyekuwa akitoa hotuba kali dhidi ya kundi la IS, ambalo baadaye lilidai kupanga shambulio lililomuuwa. Watu wasiopungua 21 walipoteza maisha katika shambulio hilo la tarehe 17 Agosti kwenye msikiti uliofurika waumini mjini Kabul.

IS bado ni changamoto kwa utawala wa Taliban

Haqqani lakini aliunga mkono elimu ya wasichana hadi kiwango cha sekondari, licha ya serikali ya Taliban kupiga marufuku wasichana kuingia darasani katika mikoa mingi ya Afghanistan.

Aghalabu kundi la IS huwalenga watu wa makundi ya wachache kama Washia, Wasufi na masingasinga. Ingawa ni kundi la madhehebu ya Suni kama walivyo Wataliban, makundi hayo ni mahasimu wakubwa, kwa sababu yanafuata itikadi tofauti za kidini.

Serikali ya Taliban hudai kuwa imelishinda kundi la IS, lakini wachambuzi wanalichukulia kundi hilo kama kitisho kikuu kwa watawala wa sasa wa Afghanistan.

-afpe, ape