Mripuko katika kituo cha makuruti Iraq
17 Agosti 2010Mripuko mkubwa ulitokea asubuhi ya leo, nje ya jengo la zamani la wizara ya ulinzi,ambalo sasa ni kituo cha kuandikisha wanajeshi katikati ya mji mkuu Baghdad. Shambulio hilo limetokea siku moja baada ya vyama viwili vikuu vya kisiasa nchini humo kuahirisha majadiliano ya kuunda serikali mpya ikiwa ni miezi mitano tangu uchaguzi kufanywa nchini humo.Afisa wa wizara ya mambo ya ndani amesema, wahanga wengi wa shambulio hilo walikuwa makuruti wa kijeshi, lakini hata baadhi ya wanajeshi waliokuwa wakilinda kituo hicho ni miongoni mwa wahanga hao.
Ahmed Kadhim, mmoja wa makuruti alienusurika katika shambulio hilo amesema, makuruti hao walikuwa wamegaiwa katika makundi mawili kwa kuzingatia sifa zao za elimu - na mshambuliaji huyo wa kujitolea muhanga alililenga lile la wahitimu wa shule ya sekondari. Akaongezea kuwa hajui mshambuliaji huyo aliwezaje kujipenyeza katika vizuizi vyote vya usalama,ambapo ilibidi avivuke, kabla ya kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo. Mripuko uliotokea katika kituo cha kuandikisha makuruti ni shambulio baya kabisa la wakati mmoja kuwahi kutokea nchini Iraq Desemba mwaka jana, wakati mfululizo wa miripuko iliyoratibiwa kwa pamoja ,ilipoua watu 127 katika mji mkuu wa Baghdad. Leo hii pia, mashambulizi mengine mawili tofauti ya mabomu dhidi ya majaji mjini Baghdad na mji wa kati wa Bakuba yamejeruhi majaji 4.
Kwa upande mwingine, mshindi wa uchaguzi mkuu wa Iraq Iyad Allawi amevunja majadiliano ya kuunda serikali ya mseto na mpinzani wake mkuu Nuri al-Maliki.Hilo ni pigo jipya kwa nchi hiyo iliyoathirika na vita.Katika tukio hilo jipya la kukatisha tamaa kwa wananchi wa Iraq wanaoteseka kutokana na kukatika kwa umeme na uhaba wa ujenzi mpya wa nchi hiyo,mshindi huyo wa uchaguzi Iyad Allawi ametaka aombwe radhi na Waziri Mkuu Nuri al-Maliki. Kwa mujibu wa msemaji wa kundi la Allawi la muungano wa vyama visivyokuwa na misimamo ya kidini, linasitisha mazungumzo na Maaliki baada ya waziri mkuu huyo katika mahojiano ya televisheni, kuliita kundi hilo kuwa ni kambi ya Wasunni. Msemaji huyo Maysoon al Damaluji amekaririwa akiliambia shirika la habari la AFP kwamba wao sio kundi la Wasunni bali ni kundi la wazalendo. Hata hivyo,kundi la Allawi limeacha mlango wazi kurejea katika mazungumzo hayo ya kuunda serikali. Lakini wamesema,bila ya kuomba radhi hawatozungumza nae tena waziri mkuu huyo.
Mwandishi:P.Martin/AFPE
Mhariri: Charo,Josephat