050810 Campbell Taylor Blutdiamanten
5 Agosti 2010Kwa muda wa miaka 11 , hadi mwaka 2002, vilizuka nchini Sierra Leone vita vya wenyewe kwa wenyewe . Sababu iliyofanya vita hivyo kuchukua muda mrefu kiasi hicho , ni biashara ya almasi ambayo ilikuwa ikitumiwa kugharamia makundi ya waasi. Charles Taylor alikuwa wakati huo rais wa nchi jirani ya Liberia. Ameshiriki katika biashara hii ya almasi na kusaidia kuendeleza vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe. Anashtakiwa kwa hiyo kwa mauaji, kuwaandikisha watoto jeshini, kusababisha ulemavu, na uporaji , katika mahakama maalum kuhusu Sierra Leone katika mji wa The Hague nchini Uholanzi.Taylor amekana mashtaka hayo . Mahakama hiyo imekuwa na wasi wasi hata hivyo kutokana na shahidi wake huyo anayefahamika sana.
Siku moja katika mwaka 1997, mrembo huyo wa kuonyesha mavazi ambaye ni maarufu duniani Naomi Campbell alihudhuria hafla iliyoandaliwa na rais wa zamani wa Afrika kusini Nelson Mandela. Katika hafla hiyo alikutana pia na kiongozi huyo wa zamani wa Liberia Charles Taylor. Taylor alivutiwa sana na uzuri wa Naomi ambapo baada ya hafla hiyo alimzawadia almasi ambazo hazijakatwa katika chumba chake cha hoteli alimofikia. Leo hata hivyo anaonna na mtu huyo aliyemhusudu lakini mara hii akiwa kizimbani katika mahakama hiyo na anatakiwa kutoa ushahidi dhidi yake.
Kesi hiyo ambayo ilianza kwa mara ya kwanza Januari 2008, ni ya kwanza kwa rais aliyekuwa akitawala barani Afrika ameweza kufikishwa mahakamani. Ni kesi inayofungua njia, kama Elly Harrowell kutoka katika shirika la kutetea haki za binadamu nchini Uingereza , Global Witness anavyoelezea.
Aina hii ya kesi inatoa ishara ya wazi, kuwa yule ambaye atafanya uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu , atafikishwa katika mkono wa sheria. Na Charles Taylor atawajibishwa kwa kile alichokifanya.
Mrembo huyo wa kuonyesha mavazi Naomi Campbell amewaambia waendesha mashtaka katika mahakama ya kimataifa kuwa alipewa almasi hizo kama zawadi nchini Afrika kusini mwaka 1997, lakini hakufahamu iwapo madini hayo ambayo yalikuwa machafu yalitolewa na rais wa zamani wa Liberia dikteta Charles Taylor.
Amesema kuwa almasi hizo alipewa zikiwa katika kisanduku cha vito katika hoteli alimofikizia na watu wawili, lakini akaongeza kuwa hakuuliza kisanduku hicho kinatoka kwa nani.
Alifungua kisanduku hicho siku ya pili, anasema. Aliona mawe machache. Yalikuwa madogo na yalionekana machafu.
Mrembo huyo amesema kuwa aliambiwa wakati wa kifungua kinywa asubuhi na mcheza sinema kutoka Marekani Mia Farrow pamoja na mshauri wake wa masuala ya mahusiano kuwa mawe hayo huenda ni ni almasi ambazo hazijakatwa ambazo huenda zimetumwa na Charles Taylor.
Mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo Brenda Hollis amesema kuwa anamatumaini ya kuthibitisha kutokana na kauli ya Campbell kuwa dikteta huyo wa zamani wa Liberia alikuwa na kile kinachoitwa almasi za damu, zilizopatikana kutoka katika maeneo ya waasi ili kugharamia ununuzi wa silaha za mamilioni ya dola kwa ajili ya Sierra Leone.
Mwandishi : Shale, Andrew / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman
E N D E