1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mradi wa nyuklia wa Iran wasonga mbele

P.Martin24 Mei 2007

Marekani inataka hatua kali zaidi zichukuliwe kuishinikiza Iran,baada ya ripoti ya shirika la IAEA kusema kuwa katika muda wa miezi michache iliyopita,Iran imezidisha takriban maradufu,idadi ya mitambo yake ya kurutubisha madini ya uranium.

https://p.dw.com/p/CHDq
Kituo cha kinyuklia nchini Iran
Kituo cha kinyuklia nchini IranPicha: picture-alliance/dpa

Kimsingi ripoti ya IAEA haikushtusha hivyo,kwani kipindi cha miezi mitatu iliyopita,Iran haikuitikia wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusita kurutubisha uranium.Badala yake, iliongeza idadi ya mitambo hadi kufikia 1312.Vile vile,hakuna ushahidi kuwa imesitisha ujenzi wa mtambo maalum unaozalisha plutonium inayoweza kutumiwa kutengenezea mabomu.Miezi hii iliyopita uchunguzi wa mitambo ya Iran uliofanywa na IAEA umepunguzwa mno.

Sasa ripoti mpya iliyowasilishwa na IAEA katika Baraza la Usalama huenda ikasababisha vikwazo vikali zaidi kuwekwa dhidi ya Iran kama Marekani inavyotoa mwito.Hata baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya sasa,zinaunga mkono mwito huo.

Tangu mgogoro wa nyuklia kuzuka hiyo miaka mitano iliyopita,Iran imeshikilia kuwa ina kila haki ya kufanya uchunguzi wa nyuklia na kuzalisha nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.Inasema,Iran haitaki zaidi ya hayo;haitaki mabomu ya nyuklia bali inataka njia nyingine ya kupata nishati na hakuna dola lolote duniani litakaloweza kuilazimisha Iran kuachilia mbali haki yake iliyo halali.Imesema,Teheran ina haki hiyo kwa sababu ya mikataba iliyokuwepo,na hasa yale makubaliano ya kutoeneza silaha za nyuklia kwa ufupi NPT.

Hata hivyo,ni dhahiri kuwa suala la Iran litafikishwa mbele ya Baraza la Usalama kwa shinikizo la Marekani na Israel hali kadhalika, kwa azma ya kuiwekea Iran vikwazo zaidi.Lakini hadi hivi sasa,yadhihirika kuwa vikwazo vilivyowekwa,havijafanikiwa.

Kinyume,ni kuwa sera hizo kali zimeufanya umma nchini Iran,kwa sehemu kubwa kushikamana na serikali katika suala la nyuklia.Si hilo tu bali hata serikali imeanza kufikiria upya ushirikiano wake na IAEA.Hata baadhi ya viongozi wanatoa wito wa kujitoa kwenye makubaliano ya NPT-kwa hivi sasa,serikali ya Teheran haitaki kwenda umbali huo.Lakini,inakataa kuheshimu makubaliano ya ziada yaliyotiwa saini kwa shinikizo la Umoja wa Ulaya.Matokeo yake ni kwamba wachunguzi wa IAEA, hawawezi tena kwenda Iran kwa ghafula na kuchagua mitambo ya kukaguliwa.