Mradi wa Al-Qaeda kuiporomosha Marekani unaonekana kufanikiwa ?
12 Septemba 2011Muongo mmoja baada ya shambulio baya lililotokea tarehe 11 Septemba dhidi ya majengo pacha ya kituo cha biashara mjini New York pamoja na wizara ya ulinzi Pentagon na licha ya kuuwawa mwanzoni mwa mwaka huu kwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda , Osama bin Laden , Al-Qaeda inaonekana kwa kiasi kikubwa kuwa imefanikiwa katika matumaini yake ya kuharakisha kuporomoka kwa nguvu za Marekani duniani, kama sio kuziweka katika ukingo wa kuvunjika kabisa.
Tathmini hiyo inaonekana kukubalika na wachambuzi wengi wa masuala ya sera za mambo ya kigeni, kukiwa na wachache tu ambao wanaamini kuwa hatua zilizochukuliwa na utawala wa rais George W. Bush zilikuwa za kupita kiasi dhidi ya mashambulio hayo na kwamba hali hiyo imeendelea hadi hii leo.
Hatua hizo za pupa zilichukuliwa kwa kiasi kikubwa na kundi lenye mafungamano ya karibu la wahafidhina maboleo pamoja na watu wengine wanaopendelea matumizi ya mabavu, ambao waliiteka sera ya mambo ya kigeni ya rais Bush hata kabla ya vumbi halijatoweka katika eneo la Lower Manhattan na kuielekeza katika mtazamo wa msimamo mkali wenye lengo la kuimarisha nguvu za Marekani katika eneo la mashariki ya kati na kuwapiga kumbo mahasimu wowote duniani ama kimkoa ambao wananyemelea kuingilia madaraka ya Marekani.
Likiongozwa kutoka ndani ya utawala huo na makamu wa rais Dick Cheney , waziri wa ulinzi Donald Rumsfeld pamoja na wasaidizi na waungaji mkono wao ambao ni wahafidhina mno , wababe hao wanaopendelea kutumia mabavu walikuwa na miaka minne kabla ya kuunganisha mradi kwa ajili ya karne mpya ya Marekani, PNAC. Ushirika huo uliasisiwa pamoja na wananadharia wa kihafidhina mamboleo William Kristol na Robert Kagan, ambao katika waraka muhimu waliouandika mwaka 1996, walitoa wito kwa Marekani kuimarisha mamlaka ya dola moja kuu dunia yaliyopatikana baada ya vita baridi kwa umbali mkubwa wa baadaye kama inavyowezekana.
Katika barua kadha pamoja na maandiko kadha , wamehimiza matumizi zaidi ya kijeshi, uingiliaji kati katika mizozo , na kama ikiwa ni muhimu, kuchukua hatua za kijeshi binafsi dhidi ya uwezekano wa vitisho, pamoja na mabadiliko ya serikali kwa mataifa yale yanayoonekana kuwa korofi, kwa kuanzia na Saddam Hussein wa Iraq.
Katika mkesha wa shambulio la Septemba 11, fikra kuwa serikali ya Marekani inaweza kupanua mamlaka yake ya kuwa dola pekee lenye nguvu duniani bila ukomo haikuonekana kuwa si kitu kisichowezekana. Ikiwa na zaidi ya asilimia 30 ya uchumi wa dunia, uwezo mkubwa wa kifedha, na bajeti ya ulinzi iliyokubwa kuliko bajeti ya kijeshi ya nchi 20 yenye nguvu kwa pamoja , Marekani ilionekana isiyoshindika, hisia ambazo zilipewa nguvu baadaye na hali ya umoja wa kitaifa iliyofuatia mashambulio hayo na kasi na urahisi ambao Marekani iliweza kuutumia katika kulishinda kundi la Taliban nchini Afghanistan baadaye mwaka huo.
Washiriki wa PNAC walifurahishwa pia. Watu wanajitokeza katika himaya ya dunia, amesema mwandishi wa makama wa gazeti la Washington Post ambaye ni mhafidhina mamboleo, Charles Krauthammer , mshabiki mkubwa wa Cheney na mtetezi wa muda mrefu wa Marekani ambayo ni nguvu pekee duniani. Ukweli ni kwamba hakuna nchi ambayo imetamalaki kiutamaduni, kiuchumi, kiteknolojia, na kijeshi katika historia ya dunia tangu himaya ya Roma.
Hamasa hiyo ni dhahiri kuwa ilichochea awamu iliyofuata katika azma ya kundi la PNAC, ambayo iliwekwa wazi katika barua iliyotumwa kwa rais Bush na ambayo iliandikwa na kundi hilo siku tisa baada ya shambulio la Septemba 11 kwa ajili ya ushindi katika kile hivi sasa kinachoitwa vita vya dunia dhidi ya ugaidi , mabadiliko ya utawala nchini Iraq.
Kushindwa kuchukua juhudi kama hizo kutasababisha kusalim amri mapema katika vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa, PNAC ilionya, wakidai kuwa Marekani ni lazima ipanue orodha yake ya malengo na kujumuisha , mataifa hususan yale ambayo yanauhasama na Israel, ambayo yanasaidia makundi ya kigaidi, pamoja na makundi yenyewe ya kigaidi.
Kwa hiyo badala ya kulenga zaidi kumkamata bin Laden na viongozi wengine wa al-Qaeda na kutoa aina ya usalama na vifaa vya msaada vinavyohitajika kuituliza Afghanistan na kuijenga upya, Bush alibadili mwelekeo , na kuelekeza nguvu za kijeshi za Marekani , katika kutayarisha vita dhidi ya Iraq. Uamuzi huo unaonekana duniani , mbali ya Cheney na waungaji wake mkono sugu wa kundi la PNAC, kuwa huenda ni uamuzi pekee ulioleta maafa katika sera za mambo ya kigeni uliochukuliwa na rais wa Marekani katika muongo mmoja uliopita, kama sio kwa karne iliyopita.
Mwandishi : Sekione Kitojo / IPS
Mhariri : Maryam Dodo Abdallah