1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye Victoire Ingabire aachiwa huru

16 Septemba 2018

Katika hatua isiyotegemewa, serikali ya Rwanda imemuachilia huru mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Victoire Ingabire, sambamba na wafungwa wengine 2,100 kupitia msamaha wa Rais Paul Kagame.

https://p.dw.com/p/34vmJ
Ruanda Entlassung aus Gefängnis | Victoire Ingabire, Opposition FDU-Inkingi
Picha: Reuters/J. Bizimana

Ingabire, aliyeachiwa Jumamosi (Septemba 15), alikuwa akitumikia kifungo cha miaka 15 jela kwa hatia za kutishia usalama wa taifa na "kuyadogosha" mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, ambayo yaliangamiza zaidi ya watu 800,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Tutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

Akiwa na uso wa tabasamu, Ingabire aliwaambia waandishi wa habari mara tu baada ya kutolewa gerezani kwamba anamshukuru Rais Kagame kwa hatua hiyo. 

"Natarajia huu uwe ni mwanzo wa kufunguka kwa uwanja wa kisiasa nchini Rwanda," alisema. Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake wa kisiasa, alisema angelitowa msimamo wake katika siku za hivi karibuni.

Mwanasiasa huyo, ambaye bado wanachama wengi wa chama chake FDU-Inkingi bado wangali jela na ambaye tangu awali alikuwa akishikilia kuwa mashitaka dhidi yake yalikuwa yamechochewa kisiasa, aliongeza kuwa: "Inaonekana serikali imegundua kuwa inaweza kufanya kazi kwa pamoja na wale wenye maoni tafauti ya kisiasa." 

Akiwa nje ya gereza alilokuwa akitumikia kifungo, Ingabire alimtolea wito Rais Kagame kuwaachia wafungwa wengine wa kisiasa.

Hatua ya kushangaza

ARCHIV Oppositionsführerin Victoire Ingabire in Ruanda festgenommen
Victoire Ingabire akipelekwa mahakamani mwaka 2011.Picha: Getty Images/AFP/S. Terril

Kuachiwa huru kwa Ingabire kuliwashangaza wengi kwa sababu ni jambo lisilo la kawaida kwa Rais Kagame, aliyehudumu kwa muda mrefu madarakani, kuwasamehe washindani wake wakubwa. 

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa magereza aliyezungumza na shirika la habari la AP kwa sharti la kutotajwa jina: "Wakati wafungwa wakijaza fomu za kuomba msamaha wa rais, wale walioshitakiwa kwa kukana mauaji ya kimbari na kula njama dhidi ya serikali huwa hawaruhusiwi kujaza fomu hizo."

Ingabire alikamatwa mwaka 2010 na kukutwa na hatia ya kupanga njama ya kuihujumu serikali na kukana mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, ambayo aliyakana, lakini akahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch liliyaita mashitaka hayo kuwa ya kisasa na kuyahusisha na ukosoaji wa mwanasiasa huyo dhidi ya serikali kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010. Serikali ya Rwanda imekuwa ikikosolewa kwa kukandamiza upinzani na kuwa na mfumo wa kisheria usio huru, shutuma ambazo inazikanusha.

Kagame anasifiwa kwa kusaidia kuubadilisha uchumi wa taifa lake, lakini pia anatuhumiwa kwa uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Mkosoaji mwengine mkubwa wa Kagame ni Diane Rwigara, ambaye bado anaendelea kusota gerezani kwa mashitaka ya kuchochea uasi na kughushi sahihi baada ya kujaribu kuwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka jana, ambao Kagame alitangazwa kushinda kwenye uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 98 ya kura. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Caro Robi