Mpatanishi wa Marekani Afghanistan ashauriana na rais Ghani
27 Januari 2019Wakati Khalilzad na mkuu wake - waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, na pia maafisa wa Taliban wakisifu maendeleo kuelekea kumaliza vita vya muda mrefu zaidi nchini Afghanistan, sasa mjumbe huyo maalum wa Marekani anapaswa kumshawishi rais Ashraf Ghani, ambaye serikali yake mpaka sasa imewekwa kando ya mchakato huo na Wataliban.
Siku sita za mazungumzo zilimalizika nchini Qatar siku ya Jumapili huku vipengelee muhimu vya makubaliano hayo vikiwa vimeainishwa, ikiwemo muda wa miezi 18 ya kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni baada ya kukamilishwa kwa makubaliano, kwa mujibu wa maafisa wa Taliban.
Rasimu hiyo pia inahusisha hakikisho kutoka kundi hilo lenye msimamo mkali kwamba halitaruhusu Aghanistan itumiwe na makundi ya Al-Qaeda na Dola la Kiislamu kuishambulia Marekani na washirika wake - sharti kuu la Marekani. Hakikisho sawa na hilo linayoyahusisha makundi mengine linatolewa kwa Pakistan katika rasimu ya makubaliano hayo.
Wataliban wanataka pia kuwa sehemu ya serikali ya muda baada ya usitishwaji wowote wa mapigano, vimesema vyanzo kutoka kundi hilo. Lakini haikuwa wazi iwapo rasimu hiyo iliyoelezwa na Wataliban inakubaliwa na pande zote au iwapo itakamilishwa na kusainiwa.
Duru mpya ya mazungumzo kati ya Khalilzad na Wataliban inatarajiwa Februari 25 mjini Doha, wamesema maafisa wawili waandamizi wa Taliban. Wakati hajahusisha moja kwa moja mpaka sasa, jukumu la rais Ghani linaweza kuongezeka wakati makubaliano kamili yakikaribia na diplomasia ikiongezeka.
Bila kufafanua kwa undani zaidi Jumamosi usiku, Khalilzad alisema katika ujumbe wa twita kwamba hakuna kinachoweza kukubaliwa bila majadiliano ya Waafghanistan wenyewe kwa wenyewe na usitishwaji kamili wa mapigano,
"Khalilzad atamfahamisha rais Ghani na maafisa wake kuhusu maendeleo, kutafuta maoni yao kabla ya kurejea Washington," afisa mwanadamizi wa Aghanistan alisema kwa sharti la kutotajwa jina. Khalilzad pia anatarajiwa kuwaarifu wanadiplomasia wa kikanda Jumatatu asubuhi.
Njia za Ghani
Wanadiplomasia wa Magharibi wanamuelezea rais Ghani kama mwebye kukabiliwa na wakati mgumu, akiwa hana mamlaka ya kuamua juu ya kuondoka kwa wanajeshi wa kigeni na uamuzi wa mwisho kutangaza usitishwaji mapigano na Wataliban.
Hata hivyo ana mamlaka ya kuamua kuunga mkono serikali ya muda kuliko kushinikiza uchaguzi wa rais ambao unaweza kuvuruga juhudi za amani. Mpaka sasa amepinga mazungumzo ya kuundwa serikali ya muda. "Ni wakati kwa Ghani kuchagua kati ya uchaguzi au mchakato wa amani," alisema mwanadiplomasia moja alieko mjini Kabul.
Licha ya maendeleo yaliofikiwa kuhusu makubaliano, vurugu zinatarajiwa kuendelea kwa nguvu, wakati ambapo Wataliban wakifanya mashambulizi ya kila siku dhidi ya serikali ya Aghanistan na vikosi vya usalama.
Wataliban wanadhibiti karibu nusu ya ardhi yote ya Afghanistan na Ghani alisema nchini Uswisi wiki iliyopita kwamba maafisa 45,000 wa vikosi vya usalama wameuawa tangu alipoingia madarakani mwaka 2014.
Kiongozi wa zamani wa Taliban alisema licha ya makubaliano kuhusu miezi 18 ya kuondoa vikosi vya kigeni, anatabiri mapigano makali huko mbele.
"Nadhani Wataliban hawataacha kupigana hadi wapate uhakika wa asilimia 100 kwamba vikosi vya kigeni vinaondoka Afghanistan," alisema Sayed Mohammad Akbar Agha, kiongozi wa kundi huru la "Ways to Save Afghanistan" ambalo linaendeshwa na viongozi wa kikabila na wasomi wa kidini wanaofanya juhudio za kusaka amani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Oummilkheir Hamidou