1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa usitishwaji mapigano Lebanon umegubikwa na nini?

27 Novemba 2024

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon ambayo yalianza kutekelezwa siku ya Jumatano, yanaweza kuvimaliza vita vilivyodumu zaidi ya mwaka mmoja lakini bado kuna wasiwasi

https://p.dw.com/p/4nUjv
Bendera ya Israel (kushoto) na ile ya Lebanon
Bendera ya Israel (kushoto) na ile ya LebanonPicha: Christian Ohde/IMAGO

Makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na Ufaransa na yaliyoanza kutekelezwa alfajiri ya jana Jumatano, na kuidhinishwa na Israel Jumanne jioni, yamejikita kwanza katika kusitisha mapigano kwa muda wa miezi miwili na kulitaka kundi la Hezbollah kuwaondoa wapiganaji wake katika eneo la kusini mwa Lebanon, huku wanajeshi wa Israel wakirejea pia nchini mwao.

Kulingana na makubaliano hayo, maelfu ya wanajeshi wa Lebanon na walinda amani wa Umoja wa Mataifa watatumwa katika eneo la kusini mwa Mto Litani ili kuimarisha usalama. Jopo la kimataifa linaloongozwa na Marekani litafuatilia katika kila upande utekelezwaji wa makubaliano hayo. Rais Biden amesema mpango huo unadhamiria kuwezesha usitishaji wa kudumu wa vita. Makubaliano hayo yanatoa fursa kwa pande zote mbili kumaliza uhasama ambao umepelekea zaidi ya Walebanon milioni 1.2 na Waisraeli 50,000 kuyahama makazi yao.

Soma pia: Israel yasitisha vita Lebanon na kuendelea kuishambulia Gaza

Maafisa wa Lebanon wanasema mashambulizi makali ya Israel huko Lebanon yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 3,700 wengi wao wakiwa raia. Pia zaidi ya watu 130 wameuawa kwa upande wa Israel. Mapigano hayo yameacha makovu kwa pande zote mbili ambapo Hezbollah imekuwa ikiishambulia Israel kwa roketi na droni, lakini Israel inaweza kudai kupata ushindi

kutokana na kumuua kiongozi mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah na makamanda wake wengine wakuu pamoja na uharibifu wa miundombinu kadhaa ya kundi hilo.

Hali ya wasiwasi yatanda

Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Pool European Pressphoto Agency/AP/dpa/picture alliance

Licha ya kufikiwa makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano, Israel imedai kuwa na haki ya kuchukua hatua ikiwa Hezbollah itakiuka makubaliano hayo, lakini maafisa wa Lebanon walikataa kuliidhinisha hilo kwenye makubaliano hayo. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema siku ya Jumanne kwamba jeshi lake litaishambulia Hezbollah ikiwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa UNIFIL, kitashindwa kutekeleza makubaliano hayo.

Mahmoud Qamati, naibu mwenyekiti wa Baraza la kisiasa la  Hezbollah ameliambia shirika la habari la Al Jazeera kuwa kundi hilo linatoa nafasi ya kuwezesha utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, lakini akasisitiza kuwa wameunga mkono mpango huo kwa sharti kwamba Israel haitaanzisha upya mashambulizi yake. Qamati amesema bila shaka wanataka kumalizika kwa "uchokozi huo" lakini si kwa gharama ya uhuru wa Lebanon.

Lakini licha ya kuwa makubaliano hayo yanaweza kutuliza mvutano huo ambao umelikumba eneo hilo, mpango huo hautoi suluhisho la moja kwa moja ili kutatua matatizo mengi hasa ya vita vya Gaza tangu lilipofanyika shambulio la Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba mwaka 2023 ambalo lilisababisha vifo vya watu 1,200.

Soma pia: Viongozi mbalimbali wapongeza makubaliano ya usitishwaji vita Lebanon

Wakati huo, kundi la Hezbollah lilianza kurusha makombora kuelekea Israel ili kudhihirisha uungwaji mkono kwa Hamas, na awali ilisema itaendeleza mapigano hayo hadi kutakapofikiwa makubaliano ya kusitishwa kwa  mapigano huko Gaza.

Lakini hatua ya Hezbollah kusitisha mapigano na Israel inaonesha ni kama kundi hilo limeshindwa kutekeleza ahadi hiyo, na hivyo kuiacha Hamas wakiwa kama yatima ambao wanatakiwa kuendeleza pekee yao vita vya kupambana na Israel. Baadhi ya watu katika kanda hiyo wanaweza kuyachukulia makubaliano ya usitishwaji mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah huko Lebanon kama ishara ya kusalimu amri.

(Chanzo: APE)