1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa usalama nchini Ujerumani kuwasilishwa

Admin.WagnerD11 Agosti 2016

Wahariri wengi wamejishughulisha zaidi leo(11.08.2016) na mpango unaotarajiwa kuwasilishwa na waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani kuhusiana na mapambano dhidi ya ugaidi hapa nchini.

https://p.dw.com/p/1JfrD
Thomas de Maiziere PK Bombenexplosion Ansbach
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de MaizierePicha: picture-alliance/dpa/M.Kappeler

Gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung , kuhusu hatua za kupambana na ugaidi hapa nchini Ujerumani. Mhariri anaandika:

"Mjadala kuhusu usalama nchini Ujerumani umeingia katika hatua ya dharura. Kuwarejesha watu makwao , kupigwa marufuku vazi la Burka ama hijabu za kujifunika uso mzima, kudhibiti na kupunguza watu kuwa na uraia wa nchi mbili, kulegeza kanuni zinazomlazimisha daktari kutoweza kutoa taarifa za mgonjwa, hiyo ndio mipango ambayo wanasiasa wa muungano unaounda serikali wanajaribu kuifanya.Hata hivyo si katika kila eneo linaonekana kuwa litapata mafanikio katika hatua hizo.Mhariri anaandika kwamba huenda ni kutokana na uchaguzi ujao ndio sababu wanasiasa wamekuja na mkakati huo.Kitu muhimu hapa ni pengine pendekezo la kuimarisha jeshi la polisi. Kwa muda mrefu kulikuwa na mahitaji makubwa ya suala hilo na utekelezaji wake. Hakuna kinachoonesha kwamba hatua hizi zimekuja baada ya msako wa kile kinachodaiwa kuwa ni Waislamu wenye itikadi kali."

Mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung kuhusu mapendekezo hayo ya waziri wa mambo ya ndani ameandika:

"Wajerumani wanatamani kwa kiasi kikubwa kuwa na usalama wa ndani. Uaminifu wao kwa wageni waliohamia katika nchi hii umeporomoka. Ndio sababu kila serikali inayoingia madarakani, ambayo inawanyooshea wakati wote wakimbizi mkono, itawalazimu iwalazimishe kufuata sheria za nchi bila kusita.

Nani ni Mjerumani ? anauliza mhariri. Na anajibu kwamba ni wale tu ambao wanatekeleza kwa dhati sheria zote za nchi na maadili yake.

Kwa kuwa tu na sheria mpya , au kuwa na sheria za kupiga marufuku, hakutaweza kumlazimisha mtu kujumuika katika jamii, kama wanavyosema wakosoaji wa mipango hiyo ya serikali ya mseto , na kwa hilo, wana haki."

USA Republikaner Donald Trump in Wilmington
Mgombea wa chama cha Republican Donald TrumpPicha: Reuters/E. Thayer

Gazeti la Der neue Tag likiandika kuhusu kampeni ya mgombea wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump , linasema; Trump anashambulia vikali kwa maneno , na zaidi ya hayo mashambulizi yana lengo lake. Matamshi yake kwamba watetezi wa sheria ya kumiliki silaha wanaweza kumsambaratisha mpinzani wake kutoka chama cha Democratic Hillary Clinton yamevuka mipaka ya mapambano ya kampeni ya uchaguzi.

Nalo gazeti la Emder Zeitung kuhusu mada hiyo , limeandika kwamba hivi karibuni walizungumza wataalamu 50 wa masuala ya usalama kutoka chama cha Trump kwamba wanajitenga na mgombea huyo. Kutokana na yale Trump anayoyasema hakuna shaka tena juu ya uelewa wa watu hawa wanaohusika na usalama wakati Trump huenda taratibu akielekea kuwa kiongozi wa nchi hiyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse

Mhariri:Caro Robi