1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa uokozi wa Dola Trilioni 1 wanukia Marekani

27 Julai 2020

Serikali ya Marekani imesema imefikia makubaliano na viongozi wa chama cha Republican katika baraza la Seneti kuhusu mpango mwingine wa dola Triolini 1 wa kusaidia kupunguza athari za janga la virusi vya corona. 

https://p.dw.com/p/3fwiN
USA Das Kapitol in Washington
Picha: Getty Imaes/AFP/C. Somodevilla

Mkuu wa Utumishi katika Ikulu ya Marekani Mark Meadows amewaambia waandishi habari kwamba anatarajia tangazo rasmi kuhusu mpango huo mpya wa uokozi litatolewa leo mchana baada ya kukamilisha masuala kadhaa yaliyohitaji marekebisho.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesema mpango huo utajumuisha nyongeza ya ruzuku kwa watu wasio na ajira ukilenga kutoa hadi asilimia 70 ya mishahara kwa watu waliopoteza kazi kutokana na janga la virusi vya corona.

Ingawa maafisa hao wawili wa serikali ya Marekani wamejizuia kutoa maelezo ziada kuhusu mpango huo, duru kutoka mjini Washington zimearifu kuwa viongozi wa Republican wanatarajiwa kuendeleza ugawaji wa fedha wa moja kwa moja kwa raia ili kupunguza makali ya kukosa ajira.

Visa vya COVID-19 vinaongezeka Marekani 

USA Präsident Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Hayo yanajiri wakati Marekani imerikodi zaidi ya maambukizi mapya 55,000 ya virusi vya corona katika muda wa saa 24 zilizopita na kufanya idadi jumla ya maambukizi nchini humo kufikia visa 4,229,624.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa idadi iliyojumuishwa na chuo kikuu cha Johns Hopkins ambazo pia zimearifu kuwa watu 518 walikufa ndani ya siku moja iliyopita na kufikisha idadi ya vifo 146,909 .

Baada ya kupungua kwa kiwango cha maambukizi mwishoni mwa msimu wa machipuko, Marekani imeshuhudia wimbi jipya la visa vya virusi vya corona zaidi katika majimbo la California, Texas, Alabama na Florida.

Ibada ya Hijja yaingia kiwingu 

Kwengineko, Saudi Arabia inajitayarisha kwa ibada ya Hijja itakayoanza rasmi Jumatano inayokuja ambayo hata hivyo itahudhuriwa na idadi ndogo ya waumini kuwahi kushuhudiwa katika historia ya miaka ya karibuni.

Saudi-Arabien einsame Pilger in Mekka an der Kaaba
Picha: AFP

Ni watu 10,000 pekee wanaoishi kwenye falme hiyo ndiyo watashiriki ibada hiyo ambayo ni moja ya nguzo za dini ya kiislamu, idadi ambayo ni ndogo mno ikilinganishwa na watu milioni 2.5 waliohudhuria Hijja mwaka uliopita.

Vyombo vya habari vya kimataifa vimepigwa marufuku kutuma wawakilishi wake wakati wa ibada ya Hijja huku serikali ya Saudia imezidisha vizuizu kwa watu kuingia kwenye mji mtukufu Makka pamoja na kuchukua hatua chungunzima za tahadhari kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona katika taifa hilo lenye zaidi ya visa vya maambukizi 260,000.

Katika hatua nyingine Vietnam imeahirisha kwa mwezi mmoja wenyeji wa mkutano wa kilele wa usalama wa kanda ya Asia ambao kwa jadi huijumuisha pia Korea Kaskazini pamoja na mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa ya jumuiya ya ASEAN kutokana na wasiwasi wa virusi vya corona.

Wanadiplomasia wawili wa Asia wamesema Vietnam ambayo mwaka huu ndiyo inaongoza Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki ya bara la Asia, ASEAN, inatumai kufanya mikutano hiyo ana kwa ana katikati ya mwezi Septemba badala ya Agosti kama ilivyopangwa hapo kabla.