Mpango wa Uganda kuhusu ARV wapingwa
3 Desemba 2013Hapo awali wanawake wajawazito waliopata maambukizi ya virusi vya ukimwi walikuwa wanatumia vidonge vya ARV kabla ya kujifungua na wakati wa kunyonyesha tu na endapo kinga yao ya mwili ikiwa imeshuka kiwango cha chini ya 350, lakini kutokana na uhaba wa mashine za kipimo hicho kwa nchi nyingi za Afrika,kutokana na bei yake kuwa juu,serikali ya uganda imeamua kupitisha matumizi ya mbinu hiyo mpya ya vidonge vya ARV kwa wanawake wajawazito,ambayo itakayowalazimu wanapoanza matibabu hayo, wasiiache kutumia vidonge hivyo katika kipindi chote cha maisha.
Hata hivyo wanaharakati wa mapambano dhidi ya ukimwi nchini humo,wakiongozwa na Dorothy Namutamba, wamepinga vikali uamuzi huo uliopitishwa na serikali wa matumitzi ya vidonge vya ARV, kwani wanadai havimpi uhuru mhusika wa kuchagua aina ya matibabu anayotaka, kwa kuwa pindi ukianza matumizi ya vidonge hivi, hupaswi kuacha,ambapo kwa wale wenye kinga za kutosha si lazima kuanza matumizi ya vidonge hivi.
Mafanikio ya mpango huo
Kutokana na mpango huo mpya wa matumizi ya vidonge vya ARV kwa wajawazito, serikali ya uganda imethibitisha mafanikio ya awali, ambapo zaidi ya asilimia 70 ya watabibu wanatumia mpango huo mpya, utakaowezesha kutimiza lengo la awali la kufikia wanawake elfu 35 kwa mwaka huu.
Mratibu wa taifa wa wizara ya Afya,kitengo cha kuzuia maambukizi ya virusi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto, bwana Godfrey Esiru,alipozungumza na shirika la habari la IPS amesema, mpaka sasa matokea ya mbinu hii ni mazuri na pia ni njia nzuri ya matibabu na nafuu sana.
Ameongeza kuwa, mojawapo ya mikakati katika mpango huo mpya wa matibabu kwa wajawazito waliopata maambukizi, kitengo chake kimetoa simu za mkononi kwa kila zahanati nchi nzima, zitakazowezesha kuratibu na kufuatilia vizuri maendeleo ya uendeshaji wa matibabu hayo kwa karibu zaidi, kwa kila zahanati.
Bwana Esiru amekiri kuwa, mpango huo unamapungufu ya kutowahusisha waume au wenzi wa wanawake wajawazito katika mpango uo mpya, na kusema kuwa wanategemea kuwatumia wanawake haohao,pamoja na waelimishaji rika, ili kuwahamasisha wanaume kuwasaidia wake zao kwenye matibabu haya.
Mjadala wazua mvutano
Mjadala huo mpaka sasa umezua mvutano kati ya wanaharakati mbalimbali, ambapo kumekuwa na makundi ya wanaopinga mpango huo na wale wanaounga mkono.Takwimu zilizotolewa na hospital ya Taifa ya mulago nchini Uganda kwa mwaka jana, zinaonyesha kuwa kati ya wanawake 190 wanaopima kiwango cha kinga mwilini, ni 20 tu kati yao wanaorudi kuchukua matokeo.
kutokana na takwimu hizo, mwanaharakati anayepinga mpango huo mbadala, bi Namutamba anafafanua kuwa kutokana na wanawake wengi walioshauriwa kupima kinga mwili ili kuanzishiwa mpango huu mpya kutorudi kuchukua matokeo yao ya vipimo, ni wazi kuwa hata matibabu yake yanakuwa vigumu kuzingatiwa na kufanya hali ya ugonjwa kuwa mbaya zaidi.
Mmoja wa wanaharakati anayeishi kwa virusi kwa miaka 20 sasa, Augustine Sebuma, anasema,kutokana na uhaba wa vipimo vilivyopo nchini, anawasiwasi na mpango huo, endapo itakuwa rahisi kujua maendeleo ya kiwango cha kinga mwili cha mhusika, ili apate ushauri wa kiafya kuwa anapaswa kuingia katika kundi lipi la matumizi ya vidonge hivyo.
Mwandishi :Diana kago/IPS
Mhariri: Saumu Yusuf