Mourinho matatani tena
28 Novemba 2016Hii ni baada ya kutimuliwa uwanjani na refarii Jon Moss wakati wa mchuano waliotoka sare ya 1-1 na West Ham. Ni mara ya tatu katika chini ya miezi miwili ambapo kocha huyo wa Manchester United atakabiliwa na hatua ya kinidhamu kutoka kwa FA.
Jose aliipa teke chupa ya maji baada ya kukasirishwa na hatua ya refarii kumwonyesha kadi nyekundu Paul Pogba kwa kujiangusha bila kuguswa na mpinzani. United wako katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Premier League na pointi 20.
Chelsea ilirejea kileleni baada ya ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Tottenham Hotspur, pointi moja mbele ya Manchester City na Liverpool ambazo zina pointi 30 kila mmoja. City walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Burnley wakati Liverpool waliwazaba Sunderland 2-0.
Arsenal ni ya nne na pointi 28 baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Bournemouth wakati Spurs wanafunga tano bora na pointi 24.
Barcelona inasuasua
Rekodi mbovu ya Barcelona katika mechi za ugenini dhidi ya Real Sociedad inaendelea baada ya mabingwa hao kukabwa kwa sare ya 1-1 hapo jana na kuteremka pointi sita nyuma ya vinara wa La Liga Real Madrid, kabla ya mcuuano wa wikendi ijayo wa ‘Classico' kati ya watani hao wa tangu jadi.
Barca sasa wako katika nafasi ya pili na pointi 27, sita nyuma ya Real Madrid ambao wana pointi 31 baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Sporting Gijon. Sevilla wanashikilia nafasi ya tatu pointi sawa na Barca baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Valencia. Atletico Madrid ni wan ne na pointi 24 baada ya kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya Osasuna. Real Sociedad wanafunga tano bora na pointi 23. Villarreal iliteremka hadi nafasi ya sita baada ya kichapo cha 2-0 dhidi ya Alaves.
Zaha aamua kuichezea Cote d'ivoire
Cote d'Ivoire imesema winga wa klabu ya Crystal Palace Wilfried Zaha, aliyeichezea England mechi mbili za kirafiki, ameamua kubadili utiifu wake wa kandanda la kimataifa na sasa ataichezea nchi hiyo ya Afrika magharibi
Tangazo hilo limekuja kabla ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ambayo yataandaliwa katikati ya msimu wa ligi kuu ya kandanda ya England hapo Januari mwakani.
Zaha mwenye umri wa miaka 24 aliichezea England mwaka wa 2012 na 2013 lakini kwa sababu michuano hiyo haikuwa ya ushindani, mchezaji huyo mzaliwa wa Abidjan anaweza kuichezea Cote d'Ivoire. Zaha alihamia London familia yake akiwa na umri wa miaka minne
FA yachunguza unyanyasaji watoto kingono
Shirikisho la kandanda la Uingereza FA limeanzisha uchunguzi kuhusiana na kashfa ya unyanyasaji watoto kingono ili kubaini kile ambacho vilabu vya kandanda vilifahamu kuhusu uhalifu uliofanywa na makocha na ni hatua gani ingepaswa kuchukuliwa kwa wakati huo.
Chama wa wachezaji wa kandanda la kulindwa kimesema zaidi ya wachezaji 20 waliwasilisha malalamiko kuhusiana na uhalifu huo. Gordon Taylor ni mwenyekiti wa chama wa wachezaji wa kulipwa. FA imesema inashirikiana kwa karibu na polisi kuhusu suala hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu