1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto umeunguza kilometa 34.2 za Mlima Kilimanjaro

28 Novemba 2022

Mamlaka ya hifadhi za taifa Tanzania TANAPA imetoa tathimini ya zoezi la uzimaji moto katika mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika, uliowaka kwa zaidi ya mwezi mmoja.

https://p.dw.com/p/4KBEO
Kenia Landschaft Kilimanjaro
Picha: Imago Images/Panthermedia/Jorge

Mamlaka ya hifadhi za taifa Tanzania TANAPA imesema kuwa madhara yaliyojitokeza ni pamoja na kuteketea kwa kilometa za mraba 34.2 za uoto wa asili ikiwepo mimea mikubwa, ambayo ni sawa na asilimia 1.9 ya eneo zima la hifadhi na hivyo kusababisha uharibifu wa maandhari ya ukanda wa juu.

Mamlaka hiyo pia imekiri kuwa teknolojia duni za uzimaji wa moto zimechangia moto huo kusambaa kwa haraka.  Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kamishina wa uhifadhi wa TANAPA Williamu Mwakilema, amebainisha kuwa haikuwa kazi rahisi kuudhibiti moto huo uliokuwa unazuka katika maeneo tofauti baada ya kudhibitiwa kutokana na sababu mbali mbali huku miongoni zikiwa ni uzoefu mdogo wa uzimaji moto katika mazingira ya mlima kwa baadhi ya wadau hasa wale ambao hawana uzoefu wa kupanda mlima na kufanya kazi kwenye maeneo ya mwinuko, ukame na upepo mkali, pamoja na teknolojia hafifu za uzimaji moto.

Kujenga hofu kwa watalii ni miongoni mwa athari za moto katika mlima Kilimajaro

Mbali na madhara ya kuteketea kwa baadhi ya eneo la misitu katika mlima huo, TANAPA imesema pia madhara mengine yaliyojitokeza ni pamoja na kujenga hofu kwa wageni pamoja na kuleta taharuki kwa watanzania na maeneo mengine duniani, kutokana na umaarufu wa mlima Kilimanjaro.

Aidha Kamishina Kalemani, amesema miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa na mamlaka hiyo katika zoezi zima la kudhibiti moto, ni ushirikiano kutoka kwa wadau mbali mbali ndani na nje ya serikali. Marry Mushi ni mwenyeji wa Moshi Kilimanjaro na mdau wa utalii, anatoa maoni yake kwa serikali ya Tanzania jinsi ya kukabiliana na majanga ya moto katika maeneo ya utalii.

Kulingana na TANAPA moto huo uliripotiwa kutokea siku ya tarehe 21 Oktoba mwaka huu 2022 majira ya saa mbili na nusu usiku katika bonde la Karanga, na baada ya kudhibitiwa ukaendelea kuzuka katika maeneo tofauti ya mlima huo ikiwapo eneo la Ubeta Samanga na Mandara karibu na Maundi Kreta.

Soma zaidi:Mtafiti wa Ujerumani angazia athari ya moto uliotokea mlima Kilimanjaro

Uchunguzi wa awali umebaini kwamba moto huo ulisababishwa na shughuli za kibinadamu mamlaka zinaendelea na uchunguzi zaidi za kuwabaini waliosababisha moto huo ili kuwachukulia hatua za kisheria. 

DW, Arusha.