MOSUL:Watu 200 wapoteza maisha Nineveh,Iraq
15 Agosti 2007Zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha yao pale shambulio la bomu lilipotokea kwenye eneo la Nineveh kaskazini mwa Iraq na kulenga madhehebu ya Yazidi.Shambulio hilo lilitokea baada ya malori manne yaliyosheheni mabomu kulipuka.Hilo ni shambulio baya zaidi kutokea na kusababisha vifo vingi kwa mpigo mmoja nchni Iraq tangu uvamizi kutokea.Maiti nyingi zinaaminika kunasa kwenye vifusi.
Wazir Mkuu wa Iraq Nuri al maliki aliwalaumu wapiganaji walio na msimamo mkali kwa kutekeleza kitendo hicho cha kihalifu.Mashambulio ya vijiji vya Al-Qathaniya na Al-Adnaniyah yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 200 na wengine 200 kujeruhiwa.Hayo ni kwa mujibu wa meya wa baraza la Sinjar Dakhil Qassim Hassun.
Kulingana na maafisa wa serikali wahanga walipekwa kwenye hospitali za eneo hilo la kaskazini huku juhudi za uokozi zikiendelea.Yapata nyumba 70 ziliporomoshwa na shambulio hilo jambo lililowafanya polisi kutangaza muda wa kutotembea kwenye eneo la Sinjar vilevile mji ulio karibu wa Tal Afar.
Marekani kwa upande wake inakashifu shambulio hilo lililoathiri maisha ya raia wasio na hatia na kuahidi kusaidia majeshi ya usalama ya Iraq kupambana na wauaji hao.
Madhehebu ya Yazidi wanaaminika kuwa na idadi ya maelfu kadhaa kote ulimwenguni na wanafuata maadili ya mwanzo ya dini ya kiislamu.Kundi hilo lina tamaduni zake maalum vilevile kuzungumza lahaja ya Kikurdi.Madhehebu ya Yazidi wanamuamini mwenyezi Mungu ..kuheshimu Quran na Biblia ila imani yao inakita zaidi kwa Malak Taus ambaye ni malaika mkuu aliye na nembo ya tausi.Wafuasi wa dini nyingi humtambua malaika huyo mkuu kama Lucifer.