1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moshi mwengine wazuka kwenye vinu vya nyuklia

23 Machi 2011

Huku wahandisi wa Kijapani wakijitihidi kuvirekebisha vinu vya nyuklia ili kudhibiti kupenya kwa mionzi yenye sumu huko Fukushima, serikali imelazimika kuwaondoa wafanyakazi wake katika eneo hilo kwa kuhofia usalama wao.

https://p.dw.com/p/10g6K
Moja ya vinu vya nyuklia vya Fukushima kikimwagiwa maji ili kukipoza
Moja ya vinu vya nyuklia vya Fukushima kikimwagiwa maji ili kukipozaPicha: Picture alliance/dpa

Shirika la Habari la Ujerumani (DPA) limeripoti kuonekana kwa moshi mzito leo hii (Jumatano, 23.03.2011), ukitoka kwenye jengo la kinu namba 3, na kusababisha wafanyakazi wa kinu hicho, wale waliokuwa kwenye kinu chengine namba 4 pamoja na wafanyakazi wa huduma za uokozi kuhamishwa kwa usalama wao.

Kamisheni ya usalama wa nyuklia ya Japan imesema hadi sasa chanzo cha moshi huo hakijajuilikana.

Kwa mujibu Shirika la Habari la Reuters, kiwango cha mionzi katika kinu hicho kilikuwa kimepanda hadi kipimo cha 435 masaa mawili kabla ya moshi kuonekana, lakini kikashuka hadi 283 baada ya moshi kuanza kufuka.

Hata hivyo, vipimo vyote viwili ni vikubwa sana, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa siku chache zilizopita.

Mbogamboga kutoka Kaginawa, Japan
Mbogamboga kutoka Kaginawa, JapanPicha: Kyodo News/AP/dapd

Hapo jana, mafundi wa Shirika la Umeme la Japan walifanikiwa kuunganisha umeme kutoka nje ya vinu vyote sita, jambo ambalo lingeliweza kuwasaidia wahandisi kuufanyia marekebisho mfumo wa kupozea mashine wa kinu namba 3.

Mionzi kwenye maji

Nako katika mji mkuu wa Tokyo, kiwango cha mionzi kinachozidi vipimo vinavyochukuliwa kuwa salama kwa watoto, kimegundulika kwenye maji ya mifereji, na kusababisha maafisa wa mji huo kuwashauri wazazi kutokuwaruhusu watoto wao kunywa maji hayo.

Hadi sasa, bado haijafahamika ni wapi hasa mionzi hii ya nyuklia inavuja, na afisa wa ngazi za juu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, James Lyon, anasema kwamba itachukuwa muda kwa ukweli hasa kujuilikana.

"Suali ni ikiwa wapi hasa mionzi hii inatoka? Je, inatoka kwenye mitambo iliyomo kwenve vinu vyenyewe au inavuja kutoka mabomba yaliyotoboka? Kwa hivyo, bila ya kwenda hasa pahala penyewe pa tukio na kufanya uchunguzi wa kina, ni shida kufahamu." Amesema Lyon.

Kugunduliwa huku kwa mionzi kwenye maji ya matumizi ya ndani mjini Tokyo, kunaongeza hofu ya wakaazi si wa mji huo tu, bali eneo zima la Japan.

Hivi sasa wataalamu wanapima hewa na maji katika maeneo mbalimbali ili kujua kiwango cha mionzi iliyozagaa tangu kuanza kuripuka kwa vinu vya Fukushima Daiichi zaidi ya wiki moja iliyopita.

Hata hivyo, likimnukuu gavana wa Tokyo, Shintaro Ishihara, Shirika la Habari la AFP linasema kwamba hadi sasa kiwango cha mionzi kilichogunduliwa mjini humo hakijakuwa na hatari kwa watu wazima.

Gavan huyo amesema kwamba wakati ni suala la tahadhari kwa wazazi kutokuwapa watoto wao maji wala maziwa ya eneo hilo, bado hakujakuwa na kitisho cha madhara ya kiafya kwa watu wengine.

Alama za kuzagaa kwa mionzi zimeonekana pia katika miji ya Gunma, Tochigi, Saitama, Chiba na Nigata.

Ofisi za kibalozi zafungwa

Wakati haya yakiendelea, imefahamika kuwa zaidi ya mataifa 25 yaliyokuwa yakiwakilishwa nchini Japan, ama yamefunga ofisi zao za kibalozi au yamehamisha makaazi yao kwa muda tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi na Tsunami zaidi ya siku kumi zilizopita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Takeaki Matsumoto, amesema kwamba manane kati ya mataifa hayo yamehamishia ofisi zao nje kabisa ya Japan.

Miongoni mwa nchi hizo ni Angola, Bahrain, Benin, Botswana, Burkina Faso, Croatia, Jamhuri ya Dominika, Ecuador, Finland, Ujerumani, Ghana, Guatemala, Kenya, Kosovo, Lesotho, Liberia, Libya, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Namibia, Nepal, Nigeria, Panama na Uswisi.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imetoa tangazo la kuwataka wafanyakazi wa ubalozi wake wanaotaka wenyewe kuondoka, kufanya hivyo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPAE
Mhariri: Othman Miraji