MOSCOW: Scheffer amtaka Putin ashirikiane na NATO
26 Juni 2007Katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi, NATO, Jaap de Hoop Scheffer, amemshauri rais wa Urusi, Vladamir Putin, ashirikiane kwa karibu na jumuiya hiyo ili kuondoa tofauti zilizopo kuhusiana na hatima ya jimbo la Kosovo na mpango wa Marekani kutaka kujenga mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora mashariki mwa Ulaya.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, ameionya jumuiya ya NATO dhidi ya mpango huo wa usalama wa Marekani uliopendekezwa kujengwa katika jamhuri ya Cheki na Poland.
Shirika la habari la Interfax limemnukulu Sergei Lavrov akisema usalama wa upande mmoja haupaswi kupuuza usalama wa upande mwingine.
Lavrov ameyasema hayo baada ya mazungumzo yake na katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jaap de Hoop Scheffer, mjini Moscow hii leo.
Sheffer amesema Urusi na jumuiya ya NATO zinatakiwa ziendelee kujadiliana kuhusu mpango huo wa usalama uliopendekezwa na Marekani na hatima ya jimbo la Kasovo nchini Serbia.