Morsi ahukumiwa kifungo cha maisha
18 Juni 2016Mahakama nchini Misri Jumamosi (18.06.2016) imemhukumu kifungo cha maisha rais wa zamani wa nchi hiyo Mohamed Morsi katka kesi ya ujasusi wakati washtakiwa wenzake sita wakihukumiwa kifo.
Wakili wake Abdel Moneim Abdel Maksoud ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mahakama hiyo ya Cairo imemfutia Morsi mashtaka ya kuipatia Qatar nyaraka za siri lakini imemhukumu kifo kwa kuliongoza kundi lililopigwa marufuku.
Qatar ilikuwa muungaji mkono mkuu wa Morsi na kundi lake la Udugu wa Kiislamu wakati kiongozi huyo alipokuwa madarakani kati ya mwaka 2012 hadi Julai 2013 alipopinduliwa na jeshi na kuwekwa mbaroni.
Morsi alikuwa amehukumiwa kifo katika kesi tafauti kutokana dhima anayodaiwa kutimiza ya wafungwa kukimbia gerezani na mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi wakati wa uasi wa mwaka 2011 uliomuondowa madarakani kiongozi aliyetawala kwa muda mrefu nchini humo Hosni Mubarak.Pia aliwahi kuhukumiwa kifungo cha maisha na kifungo cha miaka 20 gerezani katika kesi nyengine mbili tafauti.
Hukumu za kifo kwa washtakiwa sita
Mahakama hiyo pia imethibitisha hukumu za kifo dhidi ya washtakiwa wengine sita wakiwemo waandishi wa habari wawili waliokuwa wakishtakiwa bila ya wenyewe kuwepo mahakamani kwa madai ya kusaidia kuziwasilisha nyaraka hizo za siri kwa Qatar.
Waandishi hao wametambuliwa kuwa ni Ibrahim Mohamed Hilal na raia moja wa Jordan Alaa Omar ambao wote wawili ni wa kituo cha televisheni cha Al Jazeera chenye makao yake nchini Qatar.Mwandishi wa tatu ni mwanamke anayetambulika kwa jina la Asmaa Mohamed al-Khatib wa kijarida cha Raasd kinachomilikiwa na kundi la Udugu wa Kiislamu.
Washtakiwa wengine watatu waliohukumiwa kifo ni mtayarishaji wa filamu simulizi Ahmed Afifiy, mfanyakazi wa ndani ya ndege wa shirika la ndege la Misri (EgyptAir) Mohammed Keilany na mwanataaluma Ahmed Ismail.
Jaji Mohamed Shirin Fahmy amekuwa akipendekeza hukumu hiyo ya kifo kwa kipindi chote cha miezi sita iliopita.Kwa mujibu wa taratibu za Misri hukumu hizo za kifo zinatumwa kwa Mufti Mkuu wa nchi hiyo ili kuidhinishwa lakini sio lazima maoni yake yatekelezwe.
Washtakiwa ni hatari kuliko wapelelezi
Fahmy ameikariri ofisi ya mufiti ikisema washtakiwa hao sita walikuwa wakitaka kuileteya nchi madhara wakati walipotowa kwa taifa la kigeni habari kuhusu mahala wanapowekwa wanajeshi wa nchi hiyo na repoti zilizotayarishwa na mashirika ya ujasusi ya nchi hiyo.
Jaji huyo amekaririwa akisema watu hao ni hatari kuliko hata wapelelezi kwa sababu wapelelezi kwa kawaida wanakuwa raia wa kigeni wakati watu hao ni raia wa Misri waliousaliti uaminifu wao.Ameongeza kusema hakuna itikadi inayohalalisha kusalitiwa kwa nchi.
Uhusiano wa Misri na Qatar umekuwa wa mvutano tokea kupinduliwa kwa Morsi ambaye alikuwa akiungwa mkono na taifa hilo dogo la kitajiri lilioko Ghuba.Serikali ya Misri ilikuwa ikisisitiza kwamba habari za kituo cha televisheni cha Al Jazeera kuhusu Misri na kwengineko Mashariki ya Kati zimekuwa na upendeo kwa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP
Mhariri : Sylvia Mwehozi