1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mori aonya kuwa Olimpiki haifai kuahirishwa tena

23 Aprili 2020

Rais wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki Tokyo 2020 Yoshiro Mori ameonya kuwa michezo hiyo haifai kuahirishwa tena zaidi ya kipindi hiki cha mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/3bJtE
IOC Treffen in Monaco 08.12.2014 Yoshiro Mori
Picha: Reuters/E. Gaillard

Yoshiro Mori amesema hakuna nafasi ya kuahirisha michezo hiyo ambayo sasa imeratibiwa kuanza mnamo Julai 23, 2021. Mori amesema itakuwa vigumu sana kuiahirisha michezo ya Olimpiki kwa miaka miwili.

Rais huyo amedokeza kuwa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe hajapendezwa na wazo la kuiahirisha michezo hiyo kwa miaka miwili mingine. Uamuzi wa kuiahirisha michezo hiyo ya Olimpiki ulifikiwa kufuatia shinikizo kutoka kwa wanariadha na mashirika ya michezo duniani kutokana na hofu ya kusambaa kwa virusi vya Corona.

Hata hivyo, maswali yameanza kuibuka iwapo kuiahirisha michezo hiyo kwa mwaka mmoja kunatosha. Mapema wiki hii, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza katika chuo kikuu cha Kobe Kentaro Iwata amesema ana mashaka iwapo michezo hiyo itaandaliwa mwaka ujao. Iwata amesema iwapo hilo litafanikiwa, basi Japan na mataifa mengine duniani yanafaa kuja na mbinu za kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona.

Kamati andalizi ya Olimpiki ya Japan pia haijasazwa na maambukizi ya Corona kwani mmoja wa wanachama wake pia amethibitishwa kuwa na virusi hivyo. Kuahirisha michezo hiyo huenda kukaisababishia Japan hasara kubwa.

Chanzo: afp