Monti kuwania uwaziri mkuu Italia
29 Desemba 2012Tangazo lake hilo limemaliza wiki kadhaa za tetesi juu ya mustakbali wake wa kisiasa na kuondowa baadhi ya mashaka yaliokuwa yameugubika uchaguzi huo na kumuweka Monti kwenye kinyan'ganyiro cha pande tatu cha kuwania madaraka pamoja na chama cha mrengo wa kati kushoto cha Demokratik Party(PD) ambacho kinaongoza kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni na chama cha Silvio Berlusconi cha People of Freedom.Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Ulaya ambaye alichaguliwa kuongoza serikali ya wasomi mwaka jana kuiokoa Italia kutokana msukusuko wa kifedha baada ya kujiuzulu kwa Berlusconi kama waziri mkuu amesema yuko tayari kukubali kutangazwa kuwa kiongozi wa muungano huo.Monti amesema muungano huo utajaribu kupindukia mipaka ya kisiasa na kuwa na muungano mkubwa utakaounganisha makundi ya kisiasa na mashirika ya kiraia kwa agenda ya mageuzi yenye lengo la kurekebisha matatizo makubwa yalioko kwenye uchumi wa Italia.
Monti awekewa imani
Monti amekaririwa akisema kufuatia mkutano wake na wanasiasa wa mrengo wa kati akisema kwamba "Mgawanyiko wa jadi kati ya sera za mrengo wa shoto na kulia una thamani ya kihistoria na kiishara kwa nchi hiyo,lakini hakuonyeshi kuwapo kwa muungano halisi ambao Italia inauhitajia wenye kuilenga Ulaya na mageuzi."Monti ambaye ni kipenzi cha wawekezaji wa kimataifa, Kanisa Katoliki na wafanyabiashara kwa kiasi kikubwa anapongezwa kwa kuirudisha tena imani ya Italia kufuatia utawala wa miaka mingi wa Berlusconi aliejaa kashfa.Hata hivyo wananchi wa kawaida wa Italia wamezidi kuchoshwa na mpango wake wa kurekebisha mifumo ya fedha ya taifa kwa kujumuisha ongezeko la kodi na kupunguza matumizi ya serikali na uchunguzi wa maoni unadokeza kwamba asilimia 61 ya wananchi hao hawamtaki agombanie katika uchaguzi huo.
Monti ambaye hadhi yake ya kuwa seneta wa maisha ina maanisha kwamba hana haja ya kuwania kiti cha ubunge amesema kundi lao linaweza kupata matokeo mazuri katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 24 na 25 mwezi wa Februari lakini pia kumekuwepo na hofu kwamba hali hiyo inaweza kusababisha kuwepo kwa bunge dhaifu.
Uchunguzi wa maoni unadokeza kwamba chama cha PD chini ya uongozi wa Luigi Bersani kitapata ushindi wa viti vingi katika baraza la seneti lakini huenda ikabidi wafikie makubaliano na makundi ya sera za mrengo wa kati katika baraza hilo ambapo kundi hilo la sera za mrengo wa kati kushoto lilikuwa na kibaruwa kigumu kulidhibiti baraza hilo katika chaguzi zilizopita.Chama cha PD ambacho kimeahidi kuendeleza mkondo wa mageuzi wa Monti wakati kikikazania zaidi katika suala la ukuaji wa uchumi na kuzalisha nafasi za ajira kimekuwa na shaka shaka juu ya ugombea wa Monti lakini hadi sasa kimetowa kauli ya heshima kwa profesa huyo wa uchumi mwenye miaka 69.
Mashambulio ya Berlusconi
Kinyume chake Berlusconi ameanzisha kampeni ya kiwewe kwenye vyombo vya habari dhidi ya Monti kwa kile alichokiita sera za kubana matumizi za "mrengo wa wastani na Ujerumani" ambazo anazilaumu kwa kuzidi kuuzorotesha uchumi wa Italia na kuweka rekodi ya ukosefu mkubwa wa ajira.Berlusconi ameapa kufutilia mbali kodi ya mali ambayo inachukiwa na wananchi ilioanzishwa kusaidia kupunguza nakisi na mojawapo ya alama muhimu ya Monti wakati wa kipindi chake cha mwaka mmoja madarakani na pia amesema atakabiliana vilivyo na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Chama cha mrengo wa kati kushoto cha PD ambacho kimemsimamisha Piero Grasso mwendesha mashtaka wa kupambana na kundi la uhalifu la Mafia kuwa mgombea wake kimedokeza kwamba kitakuwa tayari kushiriki muungano wa Monti wa vyama vya sera za mrengo wa kati.Hata hivyo kimesema iwapo kitakuwa chama kikubwa kabisa bungeni kama vile uchunguzi wa maoni unavyodokeza kitasisitiza kutowa waziri mkuu.
Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa
Mhariri: Ssessanga,Iddi Ismail