1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU : Waislamu wadai kuteka medani ya vita

24 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCgh

Uongozi wa Kiiislam unadai kuteka medani moja ya mapambano kutoka kwa vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Ethiopia hapo jana wakati waziri mkuu wa Somalia akitahadharisha kwamba magaidi wa kigeni wamejiunga na vikosi vya Kiislam katika mapambano hayo.

Waziri Mkuu Ali Mohamed Gedi amesema wakati mapambano hayo yakipamba moto kwa siku ya nne mfululizo wapiganaji wa kigeni 4,000 wametumia fursa ya mzozo huo kujipenyeza kwenye nchi hiyo iliokosa utawala wa sheria.

Amesema hali hiyo inaonyesha jinsi magaidi wanavyozidi kujiimarisha nchini Somalia na ameitaka jumuiya ya kimataifa kufahamu kile kinachotokea nchini humo.

Wakati huo huo muungano wa Mahkama za Kiislam umerudia tena wito wao kwa Waislamu duniani kote kusaidia katika vita hivyo takatifu na kudai kwamba wameiteka medani muhimu ya mapambano ya Idale kama kilomita 60 kusini mwa makao makuu ya serikali huko Baidoa.

Mkuu wa habari wa uongozi wa Kiislam Abdurahim Ali Muddey ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wapiganaji wao wa Kiislam wameuteka mji wa Idale na kwamba wanaelekea kwenye sehemu nyengine ambapo wavamizi wa Ethiopia wamepiga kambi.

Kwa mujibu wa mashahidi pande hizo mbili zimekuwa zikishambuliana kwa mizinga,maroketi na bunduki za rashasha na kusababisha maafa makubwa.