MOGADISHU : Vikosi vya Ethiopia vyaondoka Somalia
24 Januari 2007Vikosi vya Ethiopia ambavyo vilisaidia serikali ya mpito ya Somali kuwatimuwa wanamgambo wa Kiislam vimeanza kuondoka kwenye mji mkuu wa taifa hilo la machafuko la Pembe ya Afrika hapo jana.
Generali Suem Hagoss amesema katika sherehe ya wababe wa zamani wa kivita na viongozi wa makundi kusalimisha silaha zao kwa serikali ya mpito kwamba kuanzia jana vikosi vyao vitaanza kuondoka Mogadishu.
Baadae hapo jana Wizara ya Habari ya Ethiopia ilithibitisha kwamba wanajeshi hao wameanza kuondoka.
Waziri wa mambo ya ndani wa Somalia Hussein Mohamed Farah Aideed amesema nafasi ya vikosi hivyo vya Ethiopia vyenye kuilinda serikali yake dhaifu itachukuliwa na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika AU.
Amesema wanajeshi kutoka Malawi,Uganda na Nigeria watawasili nchini humo katika kipindi kisichozidi wiki moja.
Pia amesema kwamba Afrika Kusini,Libya,Tanzania,Angola na Congo pia zimekubali kupeleka wanajeshi wake ingawa hakusema lini.