MOGADISHU : Vikosi vya Ethiopia vyakaribia Mogadishu
28 Desemba 2006Nchini Somalia vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na vikosi vya Ethiopia vinaukaribiwa mji mkuu wa Mogadishu.
Jeshi la Ethiopia limesema hapo jana kwamba halitouvamia mji mkuu huo lakini watauzingira hadi hapo vikosi vya wapiganaji wa Kiislam vitakaposalimu amri.
Waziri wa habari wa Somalia aAi Ahmed Jamah amesema watauzingira mji huo ili kutowa nafasi ya kufanyika kwa mazungumzo na kuulazimisha uongozi wa Kiislam kurudi tena kwenye mazungumzo ya amani.Amesema hivi sasa mazungumzo yanafanyika mjini humo baina ya makundi mbali mbali kuwashawishi Waislamu wenye itikadi kali kuondoka nchini Somalia kwa amani ili kuepusha maafa kwenye mji mkuu huo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi pia amesema kwamba hana utashi wa kuuteka mji wa Mogadishu.
Umoja wa Afrika na Umoja wa Waarabu wameitaka Ethiopia kuondoka vikosi vyake nchini Somalia kwa kuhofia kwamba nchi jirani zitakuja kutumbukizwa kwenye mzozo huo.
Nchini Kenya ambapo serikali yake imesaidia kuunda serikali ya mpito nchini Somalia hapo mwaka 2004 wanadiplomasia wanasema Uongozi wa Kiislam umekubali kuhudhuria mazungumzo mjini Nairobi leo hii kudhibiti hali hiyo.
Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linajiandaa kukabiliana na maelfu ya wakimbizi wa Somalia wanaotazamiwa kukimbilia katika nchi jirani za Kenya na Ethiopia.