MOGADISHU-Vikaka wa vita wasogeza wapiganaji wao vijijini kukabiliana na uvamizi wa wanajeshi wa Ethiopia.
11 Mei 2005Vikaka wa vita nchini Somalia,leo wameanza kusogeza mamia ya wapiganaji wao katika vijiji vilivyopo katikati ya nchi hiyo,kufuatia ripoti za uvamizi katika eneo hilo uliofanywa na majeshi ya Ethiopia.
Watu walioshuhudia,wamesema mamia ya watu wenye silaha na magari aina ya pick-up yaliyosheheneshwa silaha za kutungulia ndege na nyingine nzito,wameelekea katika kijiji cha Boulfulay karibu na mikoa ya Bay na Bakol nchini Somalia na kupiga kambi sehemu ambayo imeripotiwa uvamizi huo kutokea.
Mji wa Baidoa ni mji mkuu wa mikoa ya Bay na Bakol na jana kikundi cha wabunge wa Somalia,kilisema wanavijiji katika mikoa hiyo waliripoti kuwepo idadi kubwa ya watu wenye silaha,wakiwa wanasaidiwa na wanajeshi kiasi cha 500 wa Ethiopia.
Wabunge hao pia wameishutumu Ethiopia kwa kukiuka mpango wa Umoja wa Mataifa,uliodumu kwa miaka 13 wa kuingiza silaha ndani ya Somalia kwa kuvipatia silaha vikundi kadhaa vya wanamgambo.
Ethiopia inaonekana na Wasomali wengi kuwa inasaidia kuendelezwa kwa machafuko nchini mwao,kwa kuviunga mkono vikundi kadhaa vya wanamgambo wanaoipinga serikali mpya ya Somalia na Wasomali wamekuwa mstari wa mbele kupinga vikosi vya Ethiopia kujumuishwa katika jeshi la kulinda amani Somalia.