MOGADISHU: Marekani yaitetea Ethiopia kwa kuingilia kijeshi mzozo wa Somalia.
27 Desemba 2006Marekani imeitetea Ethiopia kwa kuwashambulia wanamgambo wa Kiislamu nchini Somalia lakini wakati huo huo ikaitaka serikali hiyo ichukue tahadhari ya hali ya juu inapoingilia kati mzozo huo.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani Gonzo Gallegos almesema Ethiopia ina haki ya kutetea usalama wake kutoka na hali ilivyo nchini Somalia.
Mapigano makali yalianza juma lililopita baada ya muda wa mwisho uliowekwa na wakuu wa Mahakama za Kiislamu kwa Ethiopia kuondoka nchini Somalia.
Majeshi ya Ethiopia yanayounga mkono serikali ya mpito inayotambuliwa kimataifa yamearifiwa yanazidi kusonga kuukaribi mji mkuu, Mogadishu, ambao yanasema huenda yakauteka kwa siku chache zijazo.
Mwandishi wa khabari Kadhra amesema wanamgambo wa Kiislamu nao wanajikusanya mjini ambapo hali ya hali imetanda.
Wakati Ethiopia inaposonga mbele na hujuma zake baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la nchi wanachama kumi na tano leo linatarajiwa kuendelea na mashauriano.
Wanachama wa baraza hilo waliupinga mswada uliowasilishwa na Qatar ukitaka kuondolewa majeshi yote ya kigeni, hasa majeshi ya Ethiopia.