1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Maandamano dhidi ya Ethiopia mjini Mogadishu nchini Somalia

28 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCyX

Watu kiasi ya 6,000 walijitokeza jana katika barabara za mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kwa maandamano dhidi ya Ethiopia. Mahakama za kiislamu ambazo zinaudhibiti mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, zinailaumu Ethiopia kuwapeleka maelfu ya wanajeshi kuihami serikali dhaifu ya mpito ya Somalia yenye makao yake mjini Baidoa. Ethiopia ilikiri kuwa iliwatuma nchini Somalia wataalamu wa kijeshi kuimarisha jeshi la serikali ya mpito ya Somalia lakini ilikana kuwa na wanajeshi nchini humo.

Lakini Umoja wa mataifa unahofia kutokea vita kati ya Ethiopia na Eritrea nchini Somalia katika kuwania udhibiti wa nchi hiyo. Ripoti ya siri iliotumiwa Umoja wa mataifa inasema wanajeshi kiasi ya 8,000 kutoka Ethiopia wako upande wa serikali ya mpito huku wanajeshi 2000 kutoka Eritrea wakiwa na silaha nzito, wamejiweka tayari kwa mapigano upande wa mahakama za kiislamu. Maafisa wa Umoja wa mataifa wanahofia uwezekano wa kuzuka vita kamili katika kanda nzima ya pembe la Afrika.