Mo Salah aonesha ishara nzuri za kupona
4 Juni 2018Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alikamilisha msimu ambao amekuwa na mafanikio makubwa na Liverpool, katika hali ya kukatisha tamaa wakati alipotolewa uwanjani akiwa ameumia katika nusu ya kwanza ya mchezo wa fainali ya kombe la Champions League katika kipingo dhidi ya Real Madrid mjini Kiev Mei 26 mwaka huu.
Salah alishindwa kushiriki katika mchezo wa majaribio dhidi ya Colombia Ijumaa iliyopita ambapo timu hizo zilitoka suluhu bila kufungana katika matayarisho ya Mafarao hao kutoka Afrika kaskazini katika kombe la dunia.
Misri inacheza dhidi ya Ubelgiji katika mchezo wao wa mwisho wa matayarisho siku ya Jumatano kabla ya kuanza kampeni yao ya kombe la dunia dhidi ya mahasimu wao katika kundi A , Uruguay hapo Juni 15. Wenyeji Urusi na Saudi Arabia pia wanashiriki katika kundi hilo.
Mchezaji mkongwe wa Mexico Rafael Marquez anatarajiwa kucheza michuano ya tano ya fainali za kombe la dunia baada ya kutajwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 cha nchi hiyo na kocha Juan Carlos Osorio leo Jumatatu. Mchezaji huyo wa ulinzi mwenye umri wa miaka 39 alikuwa akilengwa na wizara ya fedha ya Marekani Agosti mwaka jana kwa tuhuma za madawa ya kulenywa. Hata hivyo amepata ridhaa ya shirikisho la kandanda na atajiunga na wakongwe Antonio Carbajal, Gianluigi Buffon wa Italia na Lothar Matthaus wa Ujerumani katika kundi la wakongwe walioshiriki fainali tano wakiwa wachezaji.
Modric amsubiri Neymar Madrid
Na katika michezo ya majaribio , mlinda mlango wa Uhispania David de Gea alifanya makosa na kusababisha timu ya Uhispania kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Uswisi katika mchezo wa kujipasha joto kabla ya fainali za kombe la dunia jana Jumapili, katika mchezo ambao wenyeji Uhispania waliutawala lakini walishindwa kutumia hali hiyo kushinda.
Uhispania inasafiri kwenda katika kambi yao ya mazowezi ya Krasnodar wiki ijayo na itacheza mchezo wake wa mwisho wa kujipasha joto katika mji huo wa Urusi dhidi ya Tunisia siku ya Jumamosi, kabla ya kuwakabili mabingwa wa Ulaya Ureno katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu wa kundi B mjini Sochi Juni 15.
Mchezaji wa kati wa Real Madrid Luka Modric amemtaka nyota wa Brazil Neymar kujiunga na mabingwa hao wa Champions League baada ya kubadilishana jezi na mshambuliaji huyo kufuatia mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Brazil na Croatia jana Jumapili. Mshambuliaji huyo wa Brazil na Paris St. Germain alipachika bao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Croatia. gazeti la Uhispania la Marca liliripoti mwezi uliopita kwamba baba wa mchezaji huyo na mshauri wake , Neymar Sr. ameiambia PSG kuwa mwanae anataka kuondoka kutoka klabu hiyo haraka iwezekanavyo, akisema alikutana na wakurugenzi wa Real Madrid katika mji mkuu wa Uhispania.
Nae kocha wa zamani wa Arsenal Arsene Wenger anashauku ya kurejea tena katika kazi ya kufunza soka lakini anachukua tahadhari kabla ya kujiingiza katika changamoto ambayo atakuja juta , wakati akipana kutatua hali ya baadaye ya maisha yake katika wiki zinazokuja.
Kocha huyo wa zamani wa Arsenal aliondoka katika klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa miaka 22 mwishoni mwa msimu uliopita na hadi sasa amekuwa akihusishwa na nafasi zilizowazi za vilabu kadhaa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe /dpae
Mhariri: Josephat Charo