1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Farah kufanyiwa uchunguzi wa dawa zilizopigwa marufuku

8 Juni 2015

Data za matibabu za mwanariadha Mo Farah zitafanyiwa utathmini katika uchunguzi huru ulioamriwa na shirikisho la riadha la Uingereza. Hayo yamethibitshwa na mkuu wa riadha Uingereza

https://p.dw.com/p/1Fdcr
Leichtathletik WM Moskau Mo Farah
Picha: Reuters

Uchunguzi huo unahusu madai ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini dhidi ya kocha Mmarekani wa bingwa huyo mara mbili wa Olimpiki

Mwenyekiti wa Shirikisho la Riadha la Uingereza Ed Warner amesema leo kuwa uchunguzi huo utahusu data za damu na data nyinginezo kuhusiana na matibabu ya Farah.

USA Trainer Alberto Salazar
Kocha Mmarekani Alberto Salazar, anayemfunza Mo FarahPicha: picture-alliance/dpa/S. Dykes

Farah, Muingereza wa asili ya Kisomalia, ameapa kuendelea kufanya kazi na kocha wake Alberto Salazar hadi utakapopatikana ushahidi kuwa alihusika katika matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini. "Ikiwa madai hayo yatakuwa ya kweli, basi Alberto atakuwa amevuka mstari. Ntakuwa mtu wa kwanza kuwachana naye. Siyo vizuri. Ni kitu nilichokifanyia kazi ngumu, kwa kila kitu nilichofanikiwa maishani, na sasa jina langu linahusishwa na Alberto na bila shaka nyie mnasema tu Mo, Mo, Mo. Sio haki, sio vizuri na nina hasira kuhusu hali hii".

Farah alijiondoa katika mashindano ya riadha ya Diamond League mjini Birmingham hapo jana ili arejee Marekani kutafuta majibu ya maswali yanayomsumbua akilini. Salazar anatuhumiwa kwa kuwapa wanariadha wake virutubisho vilivyopigwa marufuku kufuatia makala iliyorushwa na televisheni ya BBC. Salazar anakanusha madai hayo

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu