Mnangagwa kuapishwa Ijumaa
22 Novemba 2017Mmoja wa wasaidizi wa Mnangagwa, Larry Mavhima amesema kuwa kiongozi huyo anarejea leo jioni na anatarajiwa kuzungumza na vyombo vya habari maara baada ya kuwasili Zimbabwe. Siku ya Jumapili Mnangagwa aliteuliwa kuwa rais wa chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF kuchukua nafasi ya Mugabe. Shirika la utangazaji la Zimbabwe limesema kuwa Mnangagwa ataapishwa siku ya Ijumaa kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo.
Jana jioni, Mugabe mwenye umri wa miaka 93, alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya urais, hatua iliyohitimisha utawala wake wa miaka 37, baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa madaraka nchini Zimbabwe kwa siku kadhaa, bila ya kumwaga damu. Jeshi hilo lilimtaka Mugabe ajiuzulu, huku akikosolewa kwa kuharibu uchumi wa nchi.
Hatua ya Mugabe kujiuzulu ilipokewa kwa shangwe kubwa na nderemo, huku Wazimbabwe wakiimba na kucheza katika mitaa mbalimbali ya nchi hiyo, kama anavyoelezea mkaazi mmoja wa Harare James Makona.
''Tuna furaha sana kuhusu jambo lote hili. Kwa sababu tumeteseka kwa muda mrefu sana. Nadhani kwa hatua hii mpya, sasa kila kitu kitakuwa sawa,'' alisema Makona.
Spika wa Bunge la Zimbabwe Jacob Mudenda ndiye aliisoma barua ya Mugabe kujizulu urais, wakati wa kikao maalum cha bunge ambacho kilikuwa kimeanza mchakato wa kisheria kumuondoa Mugabe madarakani.
Jana Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, ambaye ana uhusiano wa karibu na jeshi, ambalo lilisaidia kumuondoa Mugabe madarakani, alitangaza kuwa amekataa mualiko uliotolewa na Mugabe wa kurejea nyumbani ili kujadiliana kuhusu hali ya kisiasa katika taifa hilo. Alisema angerejea tu Zimbabwe, iwapo angehakikishiwa kuhusu usalama wake.
Mnangagwa alifukuzwa kwa utovu wa nidhamu
Mnangagwa aliyekuwa makamu wa Mugabe, alifukuzwa kazi mapema mwezi huu baada ya kutuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu na utovu wa nidhamu. Suala hilo lilichukuliwa kama njia ya kumuwezesha mke wa Mugabe, Grace Mugabe kuwa mrithi wa kiti cha urais. Inaripotiwa kuwa Mnangagwa alikimbilia nchi jirani ya Afrika Kusini, akihofia usalama wa maisha yake. Hatua ya kumfukuza Mnangagwa ilikuwa ni kosa kubwa lililofanywa na Mugabe na sasa inaonekana kuwa makamu huyo wa zamani wa rais anayejulikana kama ''Mamba,'' atarejea Zimbabwe kama mshindi.
Wakati huo huo, China imesema inauheshimu uamuzi wa Mugabe na imeahidi kuendeleza uhusiano wake wa kirafiki. China imekuwa mshirika mkubwa wa Zimbabwe kisiasa na kiuchumi kwa miaka kadhaa, baada ya mataifa ya Magharibi kumtenga Mugabe kwa tuhuma za kukiuka haki za binaadamu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lu Kang amesema kuwa nchi hiyo ina furaha kuona Zimbabwe imetatua matatizo yake kwa amani na ufanisi na kwamba sera yake kuelekea nchi hiyo haitobadilika. China imesema Mugabe amechangia kwa kiasi kikubwa katika historia ya Zimbabwe na katika harakati za ukombozi na kupata uhuru.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, amesema hatua ya Mugabe kujiuzulu inatoa fursa ya kuandaa njia mpya iliyo huru bila ya kuwepo ukandamizaji uliofanywa na utawala wa Mugabe. Kwa upande wake, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ametoa wito wa kuwepo suluhisho ambalo litaheshimu matarajio ya wananchi wa Zimbabwe kwa ajili ya ustawi wa baadae na demokrasia. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imekiita kitendo hicho kuwa cha kihistoria kwa watu wa Zimbabwe, kukomesha nchi hiyo kutengwa na kwamba mustakabali wa nchi hiyo unapaswa kuamuliwa na watu wake.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef