1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnangagwa atangaza uchaguzi Zimbabwe Julai

18 Machi 2018

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema leo kuwa uchaguzi wa kwanza wa rais na bunge nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa muda mrefu wa Robert Mugabe utafanyika mwezi Julai. Ameahidi uchaguzi wa mani na haki.

https://p.dw.com/p/2uY5W
Simbabwe Emmerson Mnangagwa in Harare, 2014
Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Uchaguzi huo utakuwa mtihani wa kwanza kwa kiongozi huyo mpya, ambaye alichukuwa madaraka mwezi Novemba baada ya jeshi kumlazimisha Mugabe mwenye umri wa miaka 94 kujiuzulu.

Pia utakuwa wa kwanza kufanyika bila jina la Mugabe kwenye karatasi ya kura tangu Zimbabwe ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1980.

"Kama taifa, chama na serikali, tunatazamia kuwa na uchaguzi wa amani, wazi na usawa mwezi Julai mwaka huu," Mnangagwa aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Jumamosi usiku.

Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, amesema uchaguzi huo hautakuwa na vurugu zilizoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita, na ambazo zilikuwa sababu ya uhusiano mbaya kati ya Zimbabwe na mataifa ya Magharibi.

Simbabwe Robert Mugabe 2008, Präsident
Rais wa zamani Robert Mugabe, ameutaja utawala wa Mnangagwa kuwa haramu na fedheha kwa Zimbabwe.Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

"Tayari nimevialika vyama vyote vya kisiasa nchini Zimbabwe kwa mazungumzo ambako sote tutajifunga kuepusha vurugu," aliongeza.

Mnangagwa atapaswa kutangaza tarehe katika tangazo rasmi. Amesema atawaalika waangalizi wa mataifa ya magharibi, waliokuwa wamepigwa marufuku wakati wa utawala wa Mugabe.

Gazeti la serikali la Sunday Mail, limesema timu ya kabla ya uchaguzi ya Umoja wa Ulaya inatarajiwa kuwasili Harare siku ya Jumatatu.

Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Zimbabwe, Phillipe Van Damme, aliliambia gazeti hilo kuwa ujumbe huo utakutana na rais, viongozi wa vyama vya siasa,pamoja na tume ya uchaguzi ya Zimbabwe.

Mugabe, katika matamshi yake ya kwanza tangu alipojiuzulu, alisema wiki iliyopita kwamba utawala wa Mnangagwa ulikuwa "haramu" na "fedheha" kwa Zimbabwe.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Sylvia Mwehozi