Mmarekani akiri kuwaua kinyama Waafghanistan
6 Juni 2013Mwanajeshi wa Marekani ameepuka kifo kwa kukiri kuwaua wanakijiji 16 nchini Afghanistan, katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mahakama ya kijeshi inayosikiliza kesi yake.
Katika mpango huo ulioratibiwa na mawakili wake, Sajent Robert Bales alikiri makosa 16 kuhusiana na mauaji ya mwaka jana kusini mwa Afghanistan, ambayo yameongeza wasiwasi katika uhusiano wa mashaka kati Marekani na Afghanistan. Jaji wa mahakama ya kijeshi Kanali Jaffery Nance alikubali maelezo hayo na kuamua kuwa Bales atakabiliwa na kifungo cha maisha jela bila kustahiki msamaha.
Aliuwa tu bila sababu
Alipoulizwa sababu za kuwaua wanakijiji hao, Bales alisema hata yeye amejiuliza swali hilo mara milioni tangu wakati huo, na kuongeza kuwa hakuna hakuna sababu yoyote anayoweza kuitoa duniani kwa kufanya mambo hayo. Bales alisema alifanya mauaji hayo kwa kutumia bubduki aina ya M4 na bastola yenye urefu wa milimita 9. Tisa kati yao walikuwa watoto. Mullah Barani anasema mdogo wake aliuawa na Bales, na sasa anamhudumia mjane na watoto wake. Yeye na manusura wengine wana hasira kwamba Bales ataepuka adhabu ya kifo.
"Walituahidi kuwa angehukumiwa adhabu ya kifo. Kama hawatasimamia ahadi yao, basi tutalaazimika kuiomba serikali yetu, rais wetu kutupatia haki. Hii ni mahakama ya upande mmoja, wamefanya uamuzi huo kwa manufaa yao na wala siyo kwa lengo la kutenda haki. Wameua mamia ya watu nchini Afghanistan, mamia wamedharaulika," alisema Mullah Barani.
Baada ya kutoa maelezo yake, Bales alisoma katika taarifa kwa sauti ya wazi na thabiti, akielezea matendo yake kwa kila mauaji. Alisema aliondoka katika kituo chake kusini mwa Afghanistan na kwenda katika vijiji vya karibu vilivyo na maboma ya udongo. Mara baada ya kuingia ndani, alisema alijenga na nia ya kuua wahanga, na baadae aliwapiga risasi moja baada ya mwingine na kisha kuchoma maiti zao, na kuongeza kuwa kitendo hicho hakikuwa na uhalali wowote wa kisheria.
Matusi kwa Afghanistan
Mauaji hayo ya mwezi Machi yaliwaghabisha raia wa Afghanistan, hasa baada ya kugundua kuwa Bales aliondolewa nchini humo. Waziri mkuu wa zamani wa Afghanistan Ahmed Shah Ahmedzai anasema mchakato wa kesi dhidi ya Bales ni matusi kwa taifa na utamaduni wa Afghanistan, na anapendekeza hata kamanda wa Bales ashtakiwa, lakini anafahamu pia kuwa uwezekano wa hilo ni mdogo sana.
"Wamerekani wamefanya matukio mengi kama hilo, lakini maskini sisi, ni nani atakaesikiliza sauti yangu, sauti yake na sauti za wale ambao wazazi wao waliuawa, hakuna, hakuna kitachotokea," alisema waziri mkuu huyo mstaafu wa Afghanistan.
Kesi ya hukumu iliyopangwa kusikilizwa tarehe 19 Agosti itaamuliwa na baraza la wajumbe 12, ambapo theluthi moja ya hao watakuwa maafisa wa jeshi. Lakini waafghanistan wengi wanahisi kuwa wamenyimwa haki ya kulipiza unyama huo, kwa kumuondolea adhanu Bales adhabu ya kifo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Josephat Nyiro Charo