1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mlipuko watikisa Mogadishu na kuua watu 20

15 Juni 2017

Watu 20 wameuawa na wengine 35 wamejeruhiwa baada ya wanamgambo kundi la Al Shabab kufanya shambulizi kwenye mikahawa miwili maarufu mjini Mogadishu.

https://p.dw.com/p/2ejyI
Somalia Restaurant Explosion
Raia wakiwa wameubeba mwili wa mtu aliyeuwawa katika mripuko MogadishuPicha: Picture alliance/AP Photo/F. Abdi Warsameh

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga alijiripua katika lango kubwa la kuingia katika mkahawa uitwao Posh Treats na hoteli katika shambulizi lililofanyika jana jioni ka kufuatiwa na makabiliano makali kati ya polisi na wanamgambo ambayo yamemalizika asubuhi ya leo. Wanamgambo watano walishambulia eneo hilo na maeneo ya jirani katika hoteli kwa kufyatua risasi jambo lililozusha hofu kubwa.

Kwa mujibu wa taarifa za walioshuhudia na polisi takribani watu wanane, wakiwemo wasichana sita waliuwawa katika kibanda cha kutengeneza chakula aina ya Pizza, wakati wengine watatu waliuwawa ndani ya mkahawa. Hata hivyo idadi nyingine ya watu waliuwawa katika mkasa huo bado haijawa wazi hadi mapema leo.

Kutapakaa kwa damu ardhini

Mteja mmoja aliyeshuhudia mkasa huo wa mauwaji katika sehemu ya mkahawa aliyetajwa kwa jina moja la Yare na shirika la habari la Ujerumani DPA amesema damu zilitapakaa katika mwili wake na kwamba vipande vya nyama vilimrukia mwilini mwake na kwamba watu walikuwa wakimzunguka katika eneo alilokaa walikuwa ama wameuwawa au wamejeruhiwa.

Somalia - Anschlag in Mogadishu
Jitihada za kusaidia majeruhi mjini MogadishuPicha: Reuters/Stringer

Aidha mgeni mwingine katika sehemu ya hoteli ya Posh Treats Olad Ahmed amesema alisikia mripuko mkubwa na kujikuta akilala chini ya meza ambapo pia pembeni yake kulikuwa na msichana aliyeuwawa. Jeshi la polisi linasema mkasa huo wa mauwaji ulitokea jana jioni ulidumu kwa masaa kadhaa.

Kauli kali ya waziri mkuu wa Somalia

Akizungumza katika radio ya umma nchini humo Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Khaire akiita kitendo hicho cha mashambulizi kuwa cha ushenzi wa kigaidi. Afisa mwingine mwandamizi idara ya usalama ya Somalia Mohammed Hassan amesema watu kadhaa wameokolewa wakiwa salama. Miongoni mwa hao wamo wageni kutoka Kenya na Ethiopia ambao walikuwa waajiliwa wa hoteli ya Posh Treats.

Kundi la waasi la Al Shabaab kupitia kituo cha radio kinachoonekana kuliunga mkono kundi hilo limeadi kuhusika na shambulizi hilo muda mfupi baada ya kutokea kwake. Kundi hilo lenye kutaka uwepo utawala wa Kiislamu nchini Somalia , linatajwa pia kuwa na mahusiano ya mtandao wa kimataifa wa kigaidi wa al Qaeda.

Kundi hilo kwa kawaida limekuwa likifanya mashambulizi katika majengo ya serikali, hoteli na mikahawa katika taifa hilo tete lililopo katika Pembe ya Afrika.  Kwa mujibu wa shirika moja lenye kuhusika na masuala ya utafiti la Marekani -Africa Center for Strategic Studies- mwaka jana ulikuwa mwaka ambao kundi la al Shabaab lilifanya matuko mengi ya mauwaji ambapo zaidi ya watu 4,200 waliuwawa.

Kundi hilo kwa hivi sasa likabaliwa na nguvu kubwa za kijeshi za Marekani baada ya Rais Donald Trump kuidhinisha upanuzi wa operesheni za kijeshi nchini humo yakiwemo ya mashambulizi ya angani. Jumapili iliyopita jeshi la Marekani barani Afrika lilisema limefanya shambulizi la angani kusini mwa Somali ambalo liliuwa wanamgambo wanane katika eneo la kuongezea mapambano na kituo cha mafunzo cha waasi.

Mwandishi: Sudi Mnette DPA/APE

Mhariri: Josephat Charo