Mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe Iran waua watu kadhaa
22 Septemba 2024Mlipuko uliosababishwa na kuvuja kwa gesi katika mgodi wa makaa ya mawe mashariki mwa Iran, umewaua watu wasiopungua 30 huku wengine zaidi ya 20 hawajulikani walipo. Ajali hiyo imetokea katika mgodi wa Tabas ulioko katika jimbo la Kusini la Khorasan. Mamlaka za jimbo hilo zimelieleza shirika la habari la Iran IRNA, kwamba timu ya uokozi inajaribu kuwaokoa wafanyakazi 22 ambao bado wamekwama.
Soma: Rais wa Iran ateua gavana wa kwanza Msunni katika miaka 45
Kulingana na shirika hilo, watu wengine 17 wamejeruhiwa wakati wa mlipuko huo, uliotokea Jumamosi wakati wafanyakazi wapatao 69 walipokuwa katika mgodi huo. Shirika la IRNA limeripoti kuwa kuvuja kwa gesi ya Methani ndiko kumesababisha mlipuko huo katika maeneo mawili ya mgodi. Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ametuma salamu za pole kwa familia za wahanga na kutaka uchunguzi ufanyike.