1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwamo waendelea kuhusu makubaliano ya CETA

Jane Nyingi
27 Oktoba 2016

EU hii leo umefuta mkutano uliokuwa umepangwa kati yake na Canada, baada ya Ubelgiji kushindwa kutatuliwa mkwamo wake wa ndani uliochelewesha kutiwa saini makubaliano ya biashara huria kati ya Umoja wa Ulaya na Canada

https://p.dw.com/p/2RlzA
CETA Kanada EU Handelsabkommen
Picha: picture-alliance/dpa/K.Ohlenschläger

Makubalino hayo maarufu kama CETA yanalenga kuondoa vikwazo vyoyote vya kibiashara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya Canada na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.Bila ya mataifa yote wanachama 28 kuzungumza kwa sauti moja,makubaliano hayo ya kibiashara hayawezi kuafikiwa.Sasa ujumbe wa Canada ukiongozwa na waziri mkuu Justin Trudeau uliokuwa usafiri Brussels kama ilivyokuwa imepangwa awali umevunja safari yake. Msemaji wa waziri wa biashara wa Canada Alex Lawrence amesema nchi yake iko tayari kutia saini makubaliano hayo muhimu pindi tu umoja wa ulaya utakuwa tayari.

Brüssel Anti TTIP CETA Demonstration
Waandamanaji wanaopinga makubaliano ya CETAPicha: picture-alliance/dpa/T. Roge

Mazungumzo ya kutatua mkwamo huo ndani ya Ubegiji yalikuwa yarejelewe leo baada ya siku kadhaa za mashauriano kutafuta makubaliano yanayoafikiwa na wahusika wote. Matumaini yalikuwa kupatikina mwafaka kwa muda unaofaa kwa mkutano wa mabalozi wa Umoja wa Ulaya baadae asubuhi ya leo.Hata hivyo waziri mkuu wa mkoa wa Wallonia Rudy Demotte amesema bado mazungumzo yataendelea. "Tumejitahidi, na naamini kila mtu amechangia pakubwa katika mazumzo hayo,lakini bado tuna maswala kadhaa yanayohitaji kutatuliwa ,na ndio sababu tupo hapa vinginevyo sisi hatungejadili." amesema Demotte

Ipo hofu mkoani Wallonia kuwa makubaliano hayo ya CETA huenda yakadhoofisha nafasi zao za kupata ajira na kuathiri viwango vya mazingira. Ipo wasiwasi pia kuwa sekta ya kilimo itaathirika pakubwa.Uhasama wa kisiasa nchini Ubelgiji kati ya viongozi wa Kisoshalisti na wale wa shirikisho la muungano wenye sera zinazoegemea upande wa kulia pia unadhaniwa kuchangia katika mkwamo uliopo kwasasa.

Sigmar Gabriel SPD Bratislava CETA
Waziri wa uchumi wa Ujerumani Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa/J.Gavlak

Waziri wa uchumi hapa ujerumani Sigmar Gabriel alisema wiki iliyopita hatazamii kutoafikiwa makubaliano hayo ya CETA,lakini itachukua muda kabla ya kujibiwa maswali yaliyotolewa na Ubelgiji na mataifa mengine. Makubalino hayo ya CETA ambayo yamekuwa yakitayarishwa kwa kipindi cha miaka saba , yanaungwa mkono na mataifa yote ya umoja wa ulaya ,lakini kupingwa kwake na eneo linalozungumza kifansa Kusini mwa Ubelgiji inaama taifa hilo kwa ujumla haliwezi kutia saini makubalino hayo. Aidha, makubalino yeyote yatakakayoafikiwa na Ubelgiji yatahitajika kuwasilishwa kwa mataifa mengine 27 ya umoja wa ulaya ili kuidhinishwa kabla ya yale ya biashara huria kati ya mataifa hayo maarufu kama CETA kutiwa saini.

Mwandishi:Jane Nyingi/RTRE/APE

Mhariri: Gakuba Daniel