Mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi Rwanda auwawa
4 Januari 2014Karegeya aliuawa katika Hotelini moja ,Afrika Kusini, ambako alikuwa akiishi uhamishoni kwa miaka kadhaa ambapo viongozi wa upinzani nchini Rwanda wamemtuhumu rais wa nchi hiyo Paul Kagame kufuatia mauaji hayo.
Kwa mujibu wa chama cha upinzani nchini Rwanda cha National Congress , Kanali Karegeya ambaye alikuwa ni rafiki wa karibu na mshirika mkubwa wa rais Kagame wakati wa vita vilivyomweka madarakani rais huyo na baadaye kumgeuka, amekutwa amenyongwa katika Hoteli ya Michelangelo, mjini Johannesburg.
Taarifa ya polisi inasema kuwa mwili wake ulipatikana kitandani ndani ya Hoteli hiyo, ambapo uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa shingo yake ilikuwa imevimba huku kukiwa na kitambaa chenye damu na kamba ndani ya chumba hicho.
Kuna kila dalili kuwa Karegeya alinyongwa na kwamba mwili wake uligundulika tarehe mosi, siku ya mwaka mpya, hivyo haijafahamika ikiwa kiongozi huyo aliuawa siku ya Jumanne au Jumatano amesema mratibu wa chama hicho cha upinzini, Theogene Rudasingwa alipozungumza kwa njia ya simu kutoka mjini Washington na kwamba, mauaji hayo yanafuatia amri iliyotolewa na rais Kagame.
Hata hivyo serikali ya rais Kagame imekana kwa nguvu tuhuma hizo, ingawa raia wa Rwanda wanaoishi uhamishoni wanasema wasimamizi wa sera kutoka Uingereza, Marekani na Ubelgiji, mara nyingi wamewaonya dhidi ya njama ya serikali kutaka kuwauwa.
Mpinzani mwingine alinusurika kuuawa mwaka 2010
Mpinzani mwingine mkubwa wa Kagame, Luteni Gegerali, Faustin Kayumba Nyamwasa alinusurika kuuawa mara mbili mwaka 2010 alipokuwa, akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa upinzani, Theogene Rudasingwa marehemu alikwenda katika Hoteli hiyo kukutana na mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Apollo, ambaye alijifanya ni rafiki wa upinzani, ambapo chumba alichokutwa amekufa kiliandikishwa kwa jina na mtu huyo, ingawa taarifa za polisi zinasema kuwa Karegeya alijiandikisha kwa jina lake katika Hoteli hiyo.
Karegeya na Nyamwasa ni miongoni mwa maafisa wakuu wanne wa zamani wa jeshi la Rwanda walioanzisha chama cha upinzani wakiwa uhamishoni miaka 6 iliyopita.
Alishushwa cheo cha Kanali 2006
Marehemu Karegeya, alitumikia kama mkuu wa ujasusi nje ya nchi kwa karibu mwongo mmoja kabla ya kushushwa cheo na kuwa msemaji wa jeshi na baadaye akakamatwa na kufungwa.
Mwaka 2006 alivuliwa cheo cha kanali na mwaka mmoja baadaye alikimbilia uhamishoni.
Yeye na wenzake bila uwepo wao mwaka 2011walihukumiwa kifungo cha muda mrefu nchini Rwanda kwa madai ya kuchochea mgawanyiko wa kikabila na kuhatarisha usalama wa nchi na uvamizi katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali. Rwanda ilitoa amri ya kukamatwa kwa viongozi hao.
Karegeya aliyekuwa na umri wa miaka 53 kwa mujibu wa Polisi, ameacha mke na watoto watatu wanaoishi mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mwandishi: Flora Nzema/APE
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman