1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa NYS akamatwa Kenya kuhusiana na ufisadi

Caro Robi
28 Mei 2018

Maafisa nchini Kenya wamemkamata mkuu wa shirika la huduma kwa vijana NYS kama sehemu ya uchunguzi kuhusu kuibiwa kwa takriban dola milioni 100 katika shirika hilo.

https://p.dw.com/p/2yRVR
Kenja Proteste gegen Korruption an Unabhängigkeitstag
Picha: picture alliance/dpa/D. Kurokawa

Vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la huduma kwa vijana NYS Richard Ndubai amekamatwa mapema leo pamoja na maafisa wengine wakiwemo mahasibu na maafisa wanaosimamia ununuzi wa vifaa NYS pamoja na wafanyabiashara waliohusika katika kandarasi na zabuni kadhaa.

Mkuu wa idara ya upelelezi amesema watu 17 wamekamatwa ili kuhojiwa kuhusiana na kashfa hiyo ya ufisadi inayoikumba NYS.

Mwendesha mkuu wa mashitaka pia amesema mashitaka dhidi ya washukiwa waliotajwa katika kashfa hiyo yataanza mara moja. Hata hivyo majina ya washukiwa hayajatolewa hadharani.

Mabilioni yapotea NYS

Vituo vya televisheni vya K24 na Citizen vimeripoti kuwa katibu wa kudumu wa wizara ya utumishi kwa umma, vijana na jinsia Lilian Mbogo Omollo amejisalilisha kwa polisi akiwa ameandamana na mawakili wake.

Kenia nach der Annulierung der Präsidentenwahl | Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya Uhuru KenyattaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Vyombo vya habari nchini Kenya katika kipindi cha majuma kadhaa sasa vimekuwa vikiripoti kuwa shilingi bilioni 10 ambazo ni sawa na dola takriban milioni 100 zimeibiwa kwa njia za kilaghai kupitia malipo ya zabuni ghushi katika shirika la huduma kwa vijana.

Shirika la Habari la Reuters halikuweza kuzungumza na Ndubai ambaye anazuiwa na polisi na pia haikuweza kuwasiliana na wakili wake.

Licha ya ahadi za mara kwa mara alizozitoa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuliongoza taifa hilo mnamo mwaka 2013 za kupambana vilivyo na ufisadi, wakosoaji wake wanamshutumu kwa kujikokota katika kuwachukulia hatua za kisheria maafisa wa ngazi ya juu serikalini wanaotuhumiwa kuhusika na ufisaidi.

Wachambuzi wanasema kushitakiwa na kufungwa kwa maafisa wakuu ndiyo njia pekee ya kukomesha jinamizi la ufisadi nchini humo.

Ufisadi wawaghadhabisha Wakenya

Ripoti hizo za kuibiwa kiasi kikubwa cha fedha katika shirika hilo la NYS, ambapo si mara ya kwanza mabilioni ya fedha kupotea katika shirika hilo, kumewaghadhabisha na kuwavunja moyo Wakenya wengi hasa ikizingatiwa kuwa mwaka 2015 NYS ilikumbwa na kashfa kama hii ya sasa, na hakuna hatua madhubiti zilichukuliwa dhidi ya watuhumiwa. Mwanaharakati Boniface Mwangi ameitisha maandamano siku ya Alhamisi wiki hii kupinga kukithiri kwa ufisadi.

Kenia Boniface Mwangi
Mwanaharakati Boniface MwangiPicha: DW/M. Braun

Jambo jingine linalowakera Wakenya ni kuwa wizi huo unatokea katika shirika linalopaswa kuwapa uwezo vijana kuwa na maarifa na kuwasaidia kupata ajira. Wiki iliyopita, wachunguzi waliwaita watu zaidi ya 40 katika idara ya upelelezi kuwahoji kuhusiana na kupotea kwa fedha hizo za NYS.

Ofisi ya mwendesha mashitaka imesema ina msingi wa kuanzisha hatua za kisheria dhidi ya washukiwa.

Rais Kenyatta amezilaumu asasi zilizotwishwa majukumu ya kupambana na ufisadi kwa kujivuta katika kupambana na ufisadi. Mwaka 2016, mkuu wa tume ya kupambana na ufisadi alisema Kenya inapoteza thuluthi moja ya bajeti yake kwa ufisadi. Hiyo inamaanisha kiasi cha takriban dola bilioni 6 hupotea kutokana na ufisaidi.

Licha ya wizara ya fedha kukanusha kuwa Kenya inapoteza kiasi kikubwa kama hicho cha fedha, Rais Kenyatta alikiri kuwa ufisadi umefikia viwango ambavyo vinatishia usalama wa kitaifa.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman