1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa kampuni ya Samsung afungwa miaka mitano jela.

25 Agosti 2017

Mahakama nchini Korea Kusini imemfunga jela miaka mitano Lee Jae-Yong bilionea wa kampuni ya simu ya Samsung. Kesi hiyo ni miongoni mwa kashfa zilizomng'oa madarakani aliyekuwa rais wa Korea Kusini, Park Geun - hye.

https://p.dw.com/p/2irE1
Südkorea Korruptionsprozess gegen Samsung-Erben Lee Jae Yong
Picha: picture-alliance/dpa/Getty Images/AP/Chung Sung-Jun

Lee Jae-Yong mwenye umri wa miaka 49 alipatikana na hatia ya kulipa rushwa ya zaidi ya dola bilioni 7.2  kwa ajili ya masomo ya mtoto wa Choi Soon-sil rafiki wa karibu wa aliyekuwa rais wa Korea Kusini Park Guen-hye na pia alitoa rushwa kwa ajili ya kupata uungwaji mkono wa serikali na pia kutaka kuwa na uwezo mkubwa wa kuidhibiti kampuni hiyo kubwa ulimwenguni inayotengeneza vifaa vya kielectroniki ya Samsung. 

Majaji watatu waliokuwa wanaisikiliza kesi hiyo walimpata Lee Jae- Yong na hatia nyingine ya kutumia vibaya fedha za kampuni ya Samsung, kuficha mali nje ya nchi na pia makosa ya uhalifu ya kuficha faida kwa kutumia vitendo vya uongo.  Waendesha mashtaka kwa upande wa serikali walitaka bilionea huyo afungwe miaka 12 jela.  Hata hivyo wakili wa bilionea huyo Sung-soo amesema hakuridhishwa na uamuzi wa mahakama na hivyo basi anapanga kukata rufaa.

Samsung Südkorea
Eneo la kuingilia katika kampuni ya SamsungPicha: picture alliance/dpa/D.Kalker

Sung - soo amesema yeye kama wakili wa kampuni ya Samsung hawezi kukubaliana na uamuzi huu wa mahakama na hasa akizingatia uamuzi katika kesi ya kwanza. wakili huyo amesema ana uhakika kwamba kesi hiyo itakaposikilizwa tena mashtaka yote dhidi ya mteja wake yatatenguliwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kusini la Yonhap, Lee alitarajiwa kuchukua nafasi ya uongozi wa kampuni ya Samsung kutoka kwa baba yake Lee Kun Hee ambaye hali ya afya sio nzuri. Taarifa kuhusu kashfa hiyo ya rushwa zilizusha maandamano ya kumshinikiza aliyekuwa rais wa Korea Kusini aachie madaraka na vurugu zilizosababisha mkuu huyo wa kampuni ya Samsung kukamatwa mnamo mwezi Februari na hatimae aliyekuwa rais wa Korea Kusini aliondolewa madarakani manmo mwezi Machi. 

Kiongozi huyo wa zamani wa Korea Kusini yumo kizuizini wakati kesi yake ikiwa bado inaendelea. Huenda akahukumiwa kifungo cha maisha iwapo atapatikana na hatia.Rafiki yake wa karibu Choi Soon-sil alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kutumia umaarufu wake kukishinikiza chuo kimoja kikuu ili binti yake apewe nafasi. Choi bado anakabiliwa na mlolongo wa mshtaka mengine. Wakurugenzi wengine wawili wa kampuni hiyo ya Samsung pia walihukumiwa kufungwa jela miaka minne kwa kuhusika katika kashfa hiyo.

 

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef