IAEA yaukaribisha uamuzi wa Iran kuhusu nyuklia
21 Novemba 2024Wakati mkutano wa bodi ya Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Nishati ya Atomiki – IAEA ulianza mjini Vienna, wanadiplomasia waliliambia shirika la habari la AFP kuwa Paris, Berlin, London na Washington ziliwasilisha rasmi muswada wa kuikemea Iran. Azimio hilo linatarajiwa kupigiwa kura Alhamisi, kwa mujibu wa wanadiplomasia. Linafuatia ziara ya mkuu wa IAEA Rafael Grossi nchini Iran, ambako pia aliyatembelea maeneo yanakofanyika shughuli kubwa za urutubishaji wa madini ya urani ya Fordo na Natanz.
Soma pia: Iran yasema iko tayari kutatua masuala yenye utata kuhusu nyuklia
Akizungumza na waandishi habari, Grossi aliikaribisha kile alichokiita "hatua thabiti” ya Iran kukubali kuweka ukomo kwenye mpango wake wa urutubishaji madini ya urani. Amesema Tehran imetekeleza hatua za maandalizi ili kuwacha kuongeza shughuli hizo.
Iran imekubali ombi la kuzingatia kurutubisha hadi asilimia 60 ya madini ya Urani na kutovuka kiwango hicho.
Lakini katika mazungumzo ya simu na Grossi, Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi alionya kuhusu kile alichokiita jibu sawa ikiwa bodi ya IAEA itapitisha azimio hilo. Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Iran IRNA. Araghchi pia amesema hatua hiyo inakinzana wazi na mazingira chanya yaliyoundwa katika mashauriano kati ya Iran na shirika hilo.
Azimio hilo linafuatia lile lililopitishwa Juni, ambalo ni Urusi na China pekee zililipinga, zikiikosoa Iran kwa kutoshirikiana na IAEA na kumuomba Grossi kutoa ripoti ya kina kuhusu shughuli za Iran.
Wanadiplomasia wanasema lengo ni kuishinikiza Iran kuingia katika mazungumzo ili kukubali vikwazo vipya dhidi ya shughuli zake za nyuklia kabla ya vile vya muafaka wa 2015 na madola yenye nguvu kufikia mwisho wake Oktoba, hata ingawa muafaka huo ulisambaratika baada ya Rais wa wakati huo Donald Trump kuiondoa Marekani katika mwaka wa 2018.
Ni mkutano wa mwisho wa robo mwaka wa bodi ya IAEA kabla ya Trump kuchukua Madaraka Januari, na bado haijafahamika kama atakubali mazungumzo ya aina hiyo.
Na kufuatia ripoti za uharibifu kwenye mpango wa nyuklia wa Iran uliosababishwa na shambulizi la Israel, Grossi ametoa wito wa sheria ya kimataifa kuheshimiwa. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliliambia bunge la Israel Jumatatu wiki hii kuwa sehemu ya mpango wa nyuklia wa Iran iliharibiwa katika shambulizi la kijeshi la Israel mwezi Oktoba. Lilikuwa la kujibu shambulizi la Iran dhidi ya Israel wiki kadhaa kabla. Grossi amesema anapanga kuzungumza na serikali ya Israel kuhusu suala hilo.
Hata hivyo Grossi amesema kuwa IAEA haizingatii eneo la Parchin nchini Iran kuwa "kiwanda cha nyuklia”. Mkuu huyo wa IAEA amewaambia waandishi kuwa hawana taarifa zozote ambazo zingethibitisha (uwepo) wa nyenzo za nyuklia" huko Parchin, ingawa eneo hilo huenda lilitumika hapo awali katika baadhi ya shughuli.
afp, dpa, reuters