1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wavunjika! Hakuna makubaliano juu ya deni la Ugiriki

Admin.WagnerD25 Juni 2015

Mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro wamemaliza mkutano bila ya kufikia makubaliano, juu ya deni la Ugiriki. Hapo awali Waziri wa fedha wa Ujerumani alisema Ugiriki ilizidi kutafautiana na wakopeshaji wake

https://p.dw.com/p/1FnRN
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: Reuters/P. Hanna

Mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro wameshindwa kufikia mapatano juu ya kuikoa Ugiriki. Mawaziri hao walikutana katika juhudi za dakika za mwisho ili kuipeusha Ugiriki kufilisika. Waziri fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble alisema hapo awali kwamba Ugiriki ilizidi kutafautiana na wadai wake.

Hata hivyo mapendekezo ya mwisho yaliwasilishwa kwa mawaziri wa fedha wa nchi za Ukanda wa sarafu ya Euro waliokutana mjini Brussels .Mapendekezo hayo yalikuwa juu ya kuipatia Ugiriki fungu la mwisho la fedha za kuiokolea nchi hiyo, lakini kwa kuyakubali masharti ya wadai wake wa Shirika la Fedha la Kimataifa,IMF,Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya ECB. Wakopeshaji wa kimataifa wanaitaka serikali ya Ugiriki ifanye mageuzi.

Waziri Mkuu Tsipras apewa muda wa mwisho

Pande hizo tatu zilimpa Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras anaefuata sera za mrengo wa kushoto muda wa hadi saa tano asubuhi leo , ili kuuwasilisha mpango thabiti wa mageuzi, ili nchi yake ipatiwe fedha. Pande hizo tatu ziliyawasilisha mapendekezo yao kwa mawaziri wa fedha wa Ukanda wa sarafu ya Euro mjini Brussels.

Rais wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro Jeroen Dijsselbloem.
Rais wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda ya Euro Jeroen Dijsselbloem.Picha: Reuters/D. Staples

Afisa mmoja mwandamizi wa Umoja wa Ulaya alisema hapo awali kwamba ikiwa Ugiriki itayakataa mapendekezo hayo basi huo ndio utakuwa mwisho.Lakini serikali ya Ugiriki imewalaumu wakopeshaji wake kwa kuyakataa maendekezo yake, ambayo hapo awali kimsingi yalikubaliwa.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema juhudi zinaendelea na huenda ikachukua muda mrefu lakini amesema anatumai mwisho wake utakuwa wa furaha.

Mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro walikutana katika juhudi za dakika za mwisho za kuleta suluhisho wakati ambapo mazungumzo baina ya Ugiriki na wakopeshaji wake wa kimataifa yamekwama.

Hapo awali Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras alikutana na wakuu wa Shirika la fedha la Kimataifa, Umoja wa Ulaya na Benki Kuu ya Ulaya.Lakini mazungumzo yao yalimalizika bila ya makubaliano. Ugiriki inatakiwa ilipe mkopo wa Shirika la fedha la kimataifa wa kiasi cha Euro Bilioni 1.6 hadi Jumanne ijayo. Lakini haitaweza kufanya hivyo bila ya kupatiwa fedha nyingine na wakopeshaji wa kimataifa.

Ikiwa haitapatiwa fedha hizo Ugiriki itashindwa kulilipa deni lake na huenda ikalazimika kujitoa kwenye Umoja wa sarafu ya Euro.

Mwandishi:Mtullya abdu/afp,rtre
Mhariri:Iddi Ssessanga